Na Happiness Shayo-TABORA
Wakuu wa Hifadhi nchini wametakiwa kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi kwa lengo la kuendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii sambamba na kuimarisha mahusiano mazuri baina yao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema hayo leo Oktoba 4,2024 Mkoani Tabora alipofanya kikao na Wahifadhi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI).
“Wakuu wa hifadhi muonane na wanakijiji muongee nao ili muwape elimu ya uhifadhi na muwashauri wawe na Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) kwenye mapori yetu ya TAWA, TANAPA na TFS” amesema Mhe. Chana.
Aidha, amewataka wahifadhi hao kuhakikisha wanaweka alama zinazoonekana katika hifadhi ili kuimarisha mipaka kwa kushirikisha Serikali za vijiji vinavyozunguka maeneo hayo.
Ameendelea kusisitiza ushirikiano kati ya taasisi hizo na taasisi zingine za kitaifa na kimataifa kwa kufanya kazi kwa pamoja katika masuala mbalimbali ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uhalifu kwenye maeneo ya hifadhi.
0 comments:
Post a Comment