Nafasi Ya Matangazo

October 08, 2024


Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amezihakikisha taasisi ya afya za kikanda na kimataifa kwamba Zanzibar inaendelea kuchukua juhudi maaluum za kudhibiti maradhi ya kuambukiza yanayowapata kinamama kipindi cha ujauzito.

Amesema, juhudi hizo zinalenga kuhakikisha ustawi wa mama na mtoto na udhibiti wa changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo Ukimwi, kifua kikuu na utapiamlo.

Mama Mariam aliyasema hayo hoteli ya Golden Tulip uwanja wa ndege, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi alipofungua Kongamano la siku tatu linajadili masuala ya afya ya mama na mtoto hususani udhibiti wa maradhi TB, HIV na Malaria linalowashirikisha wataalamu wa Afya ya mama na mtoto kutoka Kenya, Nigeria, Tanzania na Skuli ya dawa za Kitropiki ya Uingereza.

Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye idadi kubwa ya kinamama wanaojifungua, hivyo juhudi za pamoja za wadau na mashirika ya kimataifa zinahitajika kulipa kipaumbela suala la ustawi wa mama wajawazito na watoto.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inashirikiana na Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) na kwamba wataendeleza programu tofauti ambazo tayari zimeanza kuleta mafanikio ya kunusuru maisha ya mama na mtoto ili kufikia malengo yaliyomo kwenye Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2025 na ile ya dunia ya 2030.

Mama Mariam Mwinyi pia ametoa wito kwa jamii, sekta binafsi na taasisi za kimataifa kuendeleza juhudi za pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa kwa kila mdau kutimiza wajibu wake kwenye eneo lake kwa dhamira ya kuwajengea mazingira bora kinamama wakati wa ujauzito, kujifua na kuwa na uhakika maisha ya mtoto anayezaliwa.

Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazurui, amesema uwezekano wa mama kuzaa mtoto bila ya HIV, kifua kikuu na malaria unawezekana, lakini bado kuna kazi ya kufanya ili kumnusuru mtoto hasa katika utoaji wa elimu.

Amesema, Zanzibar imefanikiwa kupunguza vifo vinavyosababishwa na uzazi kwa kinamama na watoto chini ya miaka mitano, kwani hivi sasa ni vifo 12 vinavyotokea kwenye watoto 1000 wanaozaliwa na kinamama 75 wanaopoteza maisha kwenye wajawazito laki moja.

Pia, Waziri Mazurui alisisitiza, kwamba Wizara ya Afya itahakikisha inazuia, kukinga na kutibu changamoto zote zinazowakumba wajawazito, kabla na baada ya kujifungua.

Naye, daktari bingwa wa maradhi ya afya ya mama na mtoto, Dk. Salma Abdi Mahmoud ameeleza changamoto zinazowakumba kina mama wakati wa kujifungua ni pamoja na kuwa na damu kidogo, kuchelewa kupata huduma za kliniki na lishe duni.

Hata hivyo, alieleza wanaendeleza miradi mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo wahudunu wa afya134 na tayari wamepatiwa mafunzo ya afya ya mama na mtoto na tayari wana wanafunzi wanaojiendeleza kwenye skuli ya dawa za kitropiki ya Uingereza.

Kongamano hilo la siku tatu litahitimishwa kwa kutolewa ripoti ya miaka mitano ya Mradi wa Udhibiti wa Afya ya mama na mtoto na kukinga na maradhi ya TB, Ukimwi na Malaria.
Posted by MROKI On Tuesday, October 08, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo