Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa mahojiano
katika kipindi cha ‘Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo’ kinachotayarishwa na
Ofisi ya Makamu wa Rais na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
Septemba 16, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa mahojiano
katika kipindi cha ‘Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo’ kinachotayarishwa na
Ofisi ya Makamu wa Rais na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
Septemba 16, 2024. Kushoito ni Mtangazaji wa kipindi hiko, Amin Mgeni wa TBC.
***************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania
imefanikiwa kuzuia tani 216 sawa na asilimia 86 ya uzalishaji wa kemikali
hatari kwa tabaka la ozoni ambazo zingeingia nchini na kuleta madhara.
Amesema mafanikio hayo
yamekuja kutokana na Tanzania kuungana na nchi zingine duniani kuridhia na
kusaini Itifaki ya Montreal mwaka 1987 ambayo
imechangia katika hifadhi ya tabaka la ozoni.
Dkt.
Kijaji amesema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha ‘Mazingira Yetu na
Tanzania Ijayo’ kinachotayarishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kurushwa na
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Septemba 16, 2024.
Amesema
Itifaki hiyo pia imekuwa ni nyenzo muhimu katika kuchangia
jitihada
za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochangia joto duniani.
“Kabla
ya kuridhiwa kwa itifaki hii tabaka letu la ozoni lilianza kuathirika na baada
ya kuanza kutekeleza shughuli zilizomo kwenye itifaki hii iliyoridhiwa na nchi
197, tayari tumesharejesha asilimia 98 ya tabaka la ozoni na tumeshazuia tani
milioni moja nukta nane ambazo zingeingia duniani, kwenye viwanda vyetu, kwenye
shughuli za binadamu zingeendelea kumong’onyoa tabaka na dunia yetu ingekuwa
kwenye hatari kubwa,” ameeleza.
Kuhusu
jitihada za Tanzania kukabiliana na uharibifu wa tabaka la ozoni, Dkt. Kijaji
amebainisha kuwa mwaka 2007 Serikali iliandaa kanuni za kuzuia uingizaji
wa kemikali hatarishi kwa tabaka hilo na kuzifanyia maboresho mwaka 2022 ili
ziendane na wakati.
Halikadhalika, amesema kuwa
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitoa elimu kwa maafisa
katika mipaka ya nchi, bandari, forodha na viwanja vya ndege ili wazitambue
kemikali hizo na wasaidie kuzuia.
Amesema mkakati wa Serikali ni
kuhakikisha mwaka 2030 hatuhitaji kuwa na kemikali za aina hii ambapo elimu hutolewa
kwa mafundi mchundo wa kuna viyoyozi, majokofu wanapotengeneza waweze kuzuia
zisiende hewani na kuharibu tabaka la ozoni.
Hivyo, Waziri Dkt. Kijaji
ametoa wito kwa wananchi kulinda tabaka la ozoni na kwamba endapo litaharibiwa
dunia nayo itakuwa imeharibiwa na kuruhusu mionzi ya
jua kufika kwenye uso wa dunia na kusababisha
magonjwa
ya
saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na
kujikunja kwa ngozi.
Itakumbukwa Septemba 16, 2024
Tanzania iliungana na nchi zingine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya
Tabaka la Ozoni ambayo kaulimbiu kwa mwaka huu ni ‘Itifaki ya Montreal:
Kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi’.
0 comments:
Post a Comment