Nafasi Ya Matangazo

July 02, 2024






Na Happiness Shayo- Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwekezaji wa Pori la Akiba Grumeti (Grumeti Reserve), Bw. Paul Jones lengo ikiwa ni kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na  uhifadhi na utalii. Pori hilo liko katika Wilaya ya Serengeti  Mkoani Mara.

Kikao hicho kimefanyika leo Julai 2,2024 katika ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki ameishukuru kampuni ya Grumeti Reserve Ltd. kwa namna ambavyo imeendelea kujitolea katika shughuli mbalimbali za uhifadhi na utalii na kuhamasisha kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Tunashukuru kwa misaada yenu katika uhifadhi na kupambana na ujangili, lakini tunaomba msaada katika ununuzi wa vifaa zaidi kwa ajili ya Askari wa Vijiji (Village Game Scouts) ili tuweze kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na vifaa vya mawasiliano na ununuzi wa mabomu ya pilipili” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Aidha, amesema yuko tayari kushirikiana na kampuni ya Grumeti  kukabiliana na changamoto ya migogoro kati ya binadamu na  Wanyamapori katika maeneo yao.

"Tuko tayari kutoa ushirikiano katika suala hili ya ujenzi wa uzio katika eneo lenu, lakini muhimu mtoe elimu na kushirikisha wananchi ili wajue haki zao za msingi, wajue wanatoa nini na watafaidikaje" Mhe. Kairuki amesema.

Amewakaribisha wawekezaji kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya uwekezaji ikijumuisha Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA),manne (4) katika Pori la Akiba la Selous, Rungwa na Inyonga na maeneo mengine.

Katika hatua nyingine, amemtaka mwekezaji huyo kuendelea kutoa misaada kwa jamii inayozunguka eneo lake la uhifadhi, kuelimisha wananchi juu ya faida zitokanazo na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki pamoja na ufugaji nyuki ili kuongeza uzalishaji wa asali nchini ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayeweka mkazo juu ya ufugaji wa nyuki hasa kwenye kuongeza mnyororo wa thamani.

Naye, Mwekezaji wa Pori la Akiba Grumeti, Bw. Paul Jones ameiomba Serikali kutoa ushirikiano endelevu katika mchakato wa kujenga uzio katika eneo la Pori la Akiba Grumet ili kukabiliana na changamoto ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Pia, amepongeza na kushukuru kwa ushirikiano uliopo kati ya Grumeti na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kwa upande wake Kamishna Uhifadhi wa TAWA, Bw. Mabula Misungwi amewataka wawekezaji hao kushirikisha wadau wote wa uhifadhi wanapotaka  kuzungushia wakiwemo wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Kamishna Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka TANAPA, TAWA na Grumeti Reserve Ltd.
Posted by MROKI On Tuesday, July 02, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo