Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema anafurahishwa na namna makada, wanachama na
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanavyoendeleza umoja miongoni
mwao.
Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, amesema umoja miongoni mwa wanachama ndio nguzo na
silaha muhimu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Kiongozi huyo mstaafu amesema
hayo leo Jumatatu Julai 1, 2024, alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu
Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi aliyemtembelea kumjulia hali
kwenye ofisi yake binafsi, jijini Dar Es Salaam.
Rais Mstaafu Kikwete ametumia
nafasi hiyo kumwambia Balozi Nchimbi kwa jinsi anavyofurahishwa na namna
maelekezo anayotoa Mwenyekiti wa CCM Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuwataka
viongozi wa Chama kushuka chini kwa wanachama na wananchi kwa lengo la
kuwasikiliza na kutatua kero zao, yanavyotekelezwa kikamilifu.
Aidha, Rais Mstaafu Kikwete
ameipongeza sekreterieti mpya ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa jinsi
inavyojikita katika kuimarisha chama na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya 2020
-2025 kwa wananchi.
“Umoja na mshikamano wa
wana-CCM ndiyo umekuwa siri na silaha ya ushindi wa CCM, ndiyo maana tunasema
siku zote umoja wetu ndiyo ushindi wetu. Tunafurahia sana tunavyoona wana-CCM
chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan wanaendeleza kuimarisha msingi
huo. Hongereni sana," amesema Rais Mstaafu Kikwete.
Kwa upande wake, Balozi
Nchimbi amewashukuru viongozi wastaafu wa Chama na Serikali kwa jinsi
wanavyofanya kazi ya kuwalea kiuongozi na kimaadili viongozi wa sasa.
Balozi Nchimbi amesema CCM
itaendeleza utamaduni wa kuwaenzi na kuwasikiliza viongozi wastaafu.
Balozi Nchimbi amesema kwa
uzoefu wa uongozi na kazi nzuri ya kulitumikia taifa waliyofanya wakati wa
uongozi wao, viongozi hao ni hazina kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
July 01, 2024
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment