WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ushirikiano katika michezo ni nyenzo muhimu katika kudumisha diplomasia na amani miongoni mwa nchi washirika wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM).
Amesema hayo leo (Ijumaa, Mei 17, 2024) wakati akifunga Mkutano wa 79 wa Baraza hilo. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amwmwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.
“Kupitia michezo mataifa mbalimbali duniani yameweza kukuza ushirikiano na kuchangia ukuaji wa amani kwa nchi washirika”.
Amesema mikutano hiyo imekuwa ikitoa fursa kwa wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kiusalama.
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Baraza hilo kuendelea kusimamia misingi yake kwani ni muhimu katika kukuza ushirikiano na maelewano Kimataifa.
“Misingi ya baraza hili ambayo ni urafiki, mshikamano na ‘FairPlay’ sio tu inajenga misingi ya uanamichezo bali inasaidia kukuza ushirikiano wa kidiplomasia.”
Aidha, Waziri Mkuu amewashauri wajumbe wa mkutano huo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ukiwemo mlima Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment