Nafasi Ya Matangazo

April 16, 2024









Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) amewakumbusha Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuzingatia Afya sambamba na kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili kwa sababu kazi ya maokozi inahitaji nguvu na maarifa.

Mhe. Sillo ameyasema hayo leo Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana tangu kuapishwa kwake tarehe 4 Aprili, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kulipongeza kwani utendaji kazi wake unaonekana hauna kificho.

"Hongera sana Kamishna Jenerali wa Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji na Makamanda wote nimejifunza na kujua lengo kuu la kuanzishwa kwa Jeshi hili kuwa ni Kuokoa Maisha na Mali za Watanzania na hata wasio Watanzania hivyo mzingatie sana na kuweka moyoni kwamba kazi yenu ni kuwahudumia Watanzania hivyo fanyeni kazi kifua mbele kwa kujitoa kuwahudumia kwa weledi na uzalendo" Alisema Mhe. Sillo.

Mhe. Sillo amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji kuendelea kuboresha huduma  kwa Wazimamoto na Waokoaji kwa kuongeza mikakati ya kuwapatia uwezo wa mafunzo na vifaa pamoja na msaada wa kisaikolojia kwani uwekezaji katika mafunzo kwa wazimamoto na waokoaji ni jambo la msingi na halipaswi kukwepa.

Aidha Mhe. Sillo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulijengea uwezo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vitendea kazi ambavyo ndivyo vinavyo tumika katika maokozi sehemu mbalimbali.

Kupitia hotuba yake Mhe. Sillo amewapa pole Askari wote waliopata ajali ya kuungua moto wakati wakiwa katika harakati za kufanya maokozi kwenye ajali ya basi pamoja na lori la mafuta iliyotokea hivi karibuni eneo la Mlandizi Mkoani Pwani.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga, alimpongeza na kumshukuru Mhe. Sillo kwa kuonesha shauku ya kutaka kujua majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na changamoto zake.
Posted by MROKI On Tuesday, April 16, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo