Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitazama namna Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachosimamiwa
na TANESCO kinavyopokea simu na
kuhudumia wananchi wakati alipotembelea kituo hicho tarehe 4 Aprili, 2024
jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Huduma
kwa Wateja TANESCO, Martin Mwambene
akieleza namna Kituo cha Huduma kwa Wateja katika Shirika hilo kinavyopokea
simu za wananchi na kuhudumia wakati alipotembelea kituo hicho leo tarehe
4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza ripoti ya taarifa kila wiki ya Kituo cha Huduma kwa Wateja ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ianze kutolewa kila mwezi ili kufahamu maeneo yenye changamoto ya umeme nchini na kurahisisha watendaji wazembe kuchukuliwa hatua kwenye maeneo hayo.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo
wakati wa ziara kwenye kituo hicho cha huduma kwa wateja leo tarehe 4 Aprili,
2024 jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuongeza
ufanisi wa kituo hicho muhimu kwa wananchi nchini.
"Wateja wote wanaopiga
simu kwa sababu mnaletewa matatizo ya wananchi ni lazima mtengeneze kila wiki
tupate ripoti ni mkoa gani wanahudumiwa wateja kwa haraka na mkoa upi
haupewi huduma kwa haraka ili tuchukue hatua," amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameagiza kila mkoa nchini
uliopo chini ya TANESCO ufanyiwe tathmini kujua umeme umekatika mara ngapi na
kufahamu sababu zilizopelekea umeme kukatika katika maeneo hayo ili kama ni
uzembe umefanyika Serikali iweze kuchukua hatua haraka.
"Mimi ninafahamu kuna
wakati umeme unakatika sio kwa sababu ya matatizo makubwa bali ni kwa matatizo
madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini zetu. Unakuta kuna mahali mti
umedondoka kwenye njia zetu na unachukua muda mrefu kuondolewa, au mteja
amepiga simu anachukua muda kuhudumiwa, tunahitaji hiyo ripoti,"
amesisitiza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine Dkt.
Biteko ameagiza, kituo kuangalia utaratibu wa namna nzuri ya wateja
kutogharamia malipo kipindi wanapopiga simu kuhudumiwa na kituo.
"Kiu yangu ni kuona
kwamba tunakuwa na mfumo wa kupiga simu kwa Wateja bila ya kuwaingiza kwenye
gharama kwa sababu kuwaingiza kwenye gharama haina maana yoyote kwa
wanachi," ameongeza Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amemuagiza Meneja
wa Kituo hicho kuhakikisha taarifa ya Maendeleo ya kituo hicho kwa kila mkoa
inawasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati ili kuongeza ufanisi wa
watendaji nchini na asipofanya hivyo atafanyiwa mabadiliko katika kipindi
cha miezi mitatu kuanzia sasa.
Vile vile, ameagiza TANESCO
kuhakikisha inajenga taswira nzuri ya nchi kupitia watendaji wa Shirika hilo
kupitia kituo hicho. Amesema fedha zilizotolewa na Serikali za dharura kiasi
cha shilingi bilioni 2.9 watu wahudumiwe ili kufurahia kuwa Watanzania kwa
kupata huduma bora.
0 comments:
Post a Comment