Nafasi Ya Matangazo

April 07, 2024

Na Amanda Tagame, Katavi
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mha. Gissima Nyamo-Hanga amekutana na wafanyakazi wa Mkoa wa Katavi na kuwaasa kuhusu umuhimu wa kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi ya kuhudumia wananchi katika sekta ya nishati ya umeme kwani ni Shirika pekee lenye dhamana ya kutoa huduma hiyo nchini.

Ameyaeeleza hayo tarehe 06 Aprili, 2024 katika kikao alichofanya katika mkoa wa Katavi akiwa katika ziara ya kukutana na wafanyakazi katika ofisi za TANESCO Kanda ya Magharibi. 

Alianza kwa kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Katavi pamoja na wafanyakazi wote kwa juhudi kubwa wanayoifanya licha ya kuwepo na changamoto nyingi katika mkoa huo lakini wamefanikiwa kufanya kazi nzuri. Amewaasa waendelee kuchapa kazi na kuhakikisha wateja wanahudimiwa katika viwango vizuri. 

" Pamoja na changamoto zilizopo katika mkoa huu ikiwemo miundombinu mmeweza kupambana nazo niwapongeze na kuwashukuru na niwaombe muendelee zaidi ya hapo kutekeleza majukumu yenu", ameeleza Mha. Gissima. 

Ameongeza kuwa dhamana ya sekta ya nishati ya umeme iko kwa wafanyakazi wa TANESCO pekee nchini, ni wajibu wa kila mfanyakazi kuwajibika katika utendaji kazi wake ili kutimiza wajibu huo kikamilifu na kutoa huduma bora kwa Wananchi. 

" Tumekabidhiwa jukumu la kuhakikisha umeme unapatikana tuhakikishe mida wote tunaweza kuwapatia wananchi umeme nchini", amesema Mha. Gissima. 

Sambamba na hayo alisisitiza juu ya kulinda na kutunza miundombinu ya umeme na kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi kulinda mali za Shirika ili ziweze kutumika katika kuongeza ufanisi wa huduma. Amewataka viongozi kusimamia na kuhakikisha kazi zinazofanyika zinafanywa kwa viwango vinavyohitajika ili kupunguza uharibifu wa miundombinu ya umeme. 

"Hakikisheni kuwa kazi zinazofanyika mnazikagua kuwa zimefikia viwango vinavyohitajika. Pia, hakikisheni vifaa vilivyotoka stoo vimefanya kazi iliyopangiwa kikamilifu ili kupunguza upotevu wa fedha za Shirika", amesisitiza Mha. Gissima. 

Naye Meneja wa Mkoa wa Katavi Mha. Seraphine Lyimo amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kutembelea Mkoa huo kuzungumza na wafanyakazi na kuahidi kusimamia maelekezo kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu mkubwa.
Posted by MROKI On Sunday, April 07, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo