Nafasi Ya Matangazo

April 16, 2024


 Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini leo Aprili 16, 2024 imeendesha mafunzo kwa wahadhiri na wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini na wananchi ili weweze kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini.

Akimwakilisha Meneja wa Ukaguzi wa Kodi, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, CPA. Digna Bruno amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo katika Taasisi za elimu ni mkakati wa kuhakikisha wadau wa elimu wanafahamu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na kuzalisha watalaam wenye sifa zinazoendana na soko la ajira na bidhaa kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Lengo letu kama wataalam kutoka Tume ya Madini ni kuhakikisha tunasambaza elimu kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kwa wadau wa madini nchini katika sekta zote watakaoweza kujiajiri kupitia utoaji wa huduma muhimu kwenye migodi ya madini kama vile utoaji wa ushauri wa kifedha, vyakula, ulinzi na kujipatia kipato huku Serikali ikikusanya mapato yake yanayotokana na kodi mbalimbali,” amesema CPA Bruno

Naye Afisa Biashara wa Madini kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini, Issa Lunda akielezea mafanikio ya maboresho ya kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini amesema kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la ushiriki wa kampuni za kitanzania kwenye utoaji wa huduma katika migodi  ya madini sambamba na ajira kwa watanzania.

“Hapo kipindi cha nyuma, kampuni nyingi za madini zilikuwa zikiagiza hata bidhaa za kawaida kabisa nje ya nchi, lakini baada ya maboresho ya kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kampuni zinatakiwa kununua bidhaa na huduma ndani ya nchi na kuomba kibali Tume ya Madini iwapo wana mpango wa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo hazipatikani nchini,” amesema Lunda.

Katika hatua nyingine,  Lunda ameshauri vyuo vya elimu nchini kuanzisha vituo vya kutoa ushauri wa kitaalam na kushiriki kwenye utoaji wa huduma kwenye kampuni za madini, wanafunzi kuanzisha vikundi na kujiajiri kwa kutoa huduma kwenye migodi ya madini badala ya kusubiri ajira.

Aidha, ameshauri watanzania kuwekeza kwenye viwanda na kuzalisha bidhaa ambazo zinatumika kwenye migodi ya madini ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni.
Posted by MROKI On Tuesday, April 16, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo