Nafasi Ya Matangazo

March 19, 2024




Ikiwa leo ni miaka mitatu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi wamemshukuru Mhe. Rais kwa maono na maelekezo yake katika sekta za maliasili ambayo yameleta  mapinduzi makubwa katika kipindi cha uongozi wake.

Wameyasema hayo usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya maadhimisho maalum ya kumpongeza Rais Samia kwa kutimiza miaka mitatu ya uongozi wake iliyotajwa kama siku ya *"Shangwe la Utalii"* na kutaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho.

Awali, Dkt. Abbasi akiongoza timu ya majadiliano katika program maalum ya usiku wa Shangwe la Utalii kilichorushwa mbashara  na vyombo na mitandao ya kituo cha televisheni cha Clouds alielezea ujasiri na maono makubwa ya Mhe. Rais ya kuamua kucheza Filamu ya Royal Tour ambayo imeitangaza Tanzania kimataifa.

Dkt. Abbasi ndiye mwenyekiti wa kamati maalum ya Mhe.Rais ya kutangaza Tanzania ya Royal Tour.

Waziri Kairuki katika wasilisho lake maalum la takribani saa moja lililorekodiwa lilisheheni  pongezi kwa Mhe. Rais na mafanikio lukuki katika sekta za Maliasili  na Utalii na  baadaye kuhitimisha kwa kupanda jukwaani kuielezea dunia mikakati mikubwa ambayo wizara imejiwekea katika kipindi hiki.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia kumekuwa na ongezeko la bajeti ya Wizara ya Maliasili na ambapo kwa  mwaka 2021/22 ilikuwa 572,252,728,000/= mwaka 2022/23 ilikuwa 624,142,732,000/= na mwaka  2023/24 ni 654,668,208,000/= hivyo kuwezesha shughuli za utalii na uhifadhi.

Kuhusiana na ongezeko la watalii na mapato katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Mhe. Kairuki amesema 2023 watalii wa kimataifa walifikia 1,808,205 sawa na ongezeko la asilimia 191 ikilinganishwa na watalii 620,867 mwaka 2020 na mapato yatokanayo na shughuli za utalii kuongezeka ambapo mwaka 2023 mapato yalifikia Dola za Marekani Bilioni 3.3 sawa na ongezeko la asilimia 371 ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 0.7 mwaka 2020.

Katika  Sekta ya Wanyamapori, Waziri Kairuki amesema Tanzania imeongoza Afrika na Duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya Wanyamapori kutokana na kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kudhibiti ujangili wa wanyamapori hususani tembo, simba na nyati.

Amefafanua kuwa pia Serikali imeendelea kutatua migogoro ya ardhi baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa ambapo Rais Samia amemega sehemu ya Hifadhi za Misitu 38, Mapori ya Akiba na Tengefu 15, Hifadhi za Taifa 7 na Eneo moja la Malikale na kuwarejeshea kwa wananchi wa vijiji 251. Hatua hii imewezesha wananchi katika vijiji husika kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji hivyo kustawisha maisha yao.

Kuhusiana na Sekta ya Misitu na Nyuki, Mhe. Kairuki amesema kuwa jumla ya misitu mipya 55 yenye ukubwa wa hekta 1,453,025.846 ilianzishwa na kutangazwa kupitia Gazeti la Serikali (GN) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilizalisha jumla ya tani 67,523 za mbegu za miti na kuotesha miche 97,544,879 ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa katika mashamba 24 ya Serikali na mingine kugawiwa kwa watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao. 

Ameweka bayana kuwa Serikali imeongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini hadi kufikia wastani wa tani 32,691 kutoka tani 31,179 sawa na ongezeko la asilimia 5% ambapo Tanzania imeuza jumla ya tani elfu 5.6 za asali   nje ya nchi yenye thamani ya Dola za Marekani   milioni arobaini (40, 000,000/=). 

Katika kuhakikisha kwamba Wizara hiyo inaendelea kuongeza mapato Serikali imeimarisha mifumo ya kitaasisi kwa ajili ya kusimamia sekta ya Malikale ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sheria ya Mambo ya Kale Sura 233 na Sheria ya Makumbusho Sura 280 ili kuzipa nguvu ya kisheria kuratibu na Kusimamia uhifadhi, uendelezaji na uboreshaji wa Maeneo ya Malikale na makumbusho za Taifa ipasavyo ambapo katika kipindi cha uongozi wa miaka mitatu ya Rais Samika Serikali imefungua maeneo mapya na kujenga vituo vya taarifa na miundo mbinu ya kiutalii katika maeneo ya Mbuamaji, Kigamboni; Mikumbi na Tendaguru Lindi Mjini. 

Waziri Kairuki amewahakikishia wadau wote wa Sekta ya Maliasiili na Utalii kwamba  Wizara hiyo itaendelea kusimamia maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza utalii na kuibua mazao mapya ya utalii, kulinda wanyamapori kwa faida ya uhifadhi na uchumi, kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji, kuboresha miundombinu kwenye maeneo yetu mbalimbali ya kiutalii na  kulinda Sekta ya Misitu na Nyuki.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava alisema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia kuundwa kwa mfuko wa maendeleo ya utalii utakaochangiwa na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinazokusanya mapato.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe  19 /03/2021  anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake  tangu alipokabidhiwa madaraka tarehe 19/03/2021.
Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo