Nafasi Ya Matangazo

April 21, 2024








Na Mwandishi Wetu, Singida
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ameagiza kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wanafunzi wa kike waliopata mimba wakiwa shuleni wakiwemo wazazi kama hatua ya kukomesha tatizo hilo ambayo limeonekana kuwa ni kero kubwa katika maendeleo ya sekta elimu mkoani SINGIDA.

Mkuu huyo wa mkoa wa SINGIDA ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti (leo 21-Apr-2024) katika ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili katika Halmashauri ya wilaya ya Itigi wakati anakagua ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na kuzugumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini ITIGI ili kutatua kero zinazowakabili.

Mkuu wa mkoa wa SINGIDA amesema ili kukomesha tatizo hilo yeye ataanza kukamata kwanza msichana aliyepata mimba na baadaye mvulana ambaye atakuwa mtuhumiwa namba mbili kama hatua ya kukomesha vitendo vya mimba kwa wanafunzi.

“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshtakiwa namba Moja na wewe ndio utakayeenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko kwa sababu mna tabia ya ukipata mimba tunaenda kukimbizana na mtoto wa kiume si sawa wote mlishirikiana kwa hiyo yeye atakuwa mstakiwa namba mbili na msichana atakuwa mstakiwa namba Moja,” Amesisitiza Halima Dendego.

Kuhusu wanafunzi 4,000 kutoripoti shuleni mkoani Singida hadi sasa, Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ametoa muda wa mwezi Mmoja kwa Makatibu Tarafa na Maafisa Watendaji wa Vijiji na kata wahakikishe wanawasaka wanafunzi hao popote walipo na kuwarudisha shuleni vinginevyo watakiona cha moto.

Amesema itakuwa jambo la aibu kwa Serikali kujenga shule kwa gharama kubwa huku wanafunzi wanaotakiwa kusoma kwenye shule hizo hawapo shuleni na kusisitiza kuwa hatakubali hata kidogo aibu hiyo imkute na ni lazima wanafunzi hao wasakwe popote walipo ili warudishwe shuleni wakasome.

Halima Dengedo ameagiza kupatiwa taarifa zote za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao hawajaripoti shuleni mpaka sasa hata kama wamehama na shule walipohamia ili aweze kufutia kama ni kweli yupo kwenye shule hiyo au ni uongo. 

Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt Fatma Mganga amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa mfano kwa wazazi na jamii nzima na kuachana na mambo yanaenda kinyume cha maadili ya Kitanzania.

Fatma Mganga amesema kuwa kama wanafunzi watasoma kwa bidii hadi Vyuo Vikuu watakuwa na faida kubwa sio tu kwa familia zao bali kwa jamii nzima na Taifa kwa ujumla kwa sababu Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Posted by MROKI On Sunday, April 21, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo