Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewaasa wazazi na walezi kuwajengea watoto uwezo wa kujitambua na kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia kufuatia hatari ya matukio ya ukatili na unyanyasaji yanayoendelea katika jamii.
Ni katika viwanja vya 'Nyerere square' Jijini Dodoma ulipofanyika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia leo Novemba 30/2023.
"Nitumie fursa ya kampeni hii ya siku 16 kuwakumbusha wazazi/ walezi na jamii kuwajengea watoto wetu uwezo ili waweze kujitambua na kujilinda dhidi ya matukio ya ukatili kwani watoto Wapo katika hatari zaid ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.
"Nitoe rai kwa watendaji katika ngazi mbalimbali kuhakikisha kunakuwa na mifumo ya utoaji wa msaada wa haraka pale inapobainika mtu amefanyiwa ukatili wa kijinsia ili manusura awezeshwe kupata huduma kwa haraka kuepusha athari zaidi," amesema Senyamule
Aidha Senyamule ametaja maeneo ya kupeleka taarifa ikiwa mtu amefanyiwa ukatili ni Kituo cha huduma za Afya, Dawati la jinsia na watoto kwenye jeshi la polisi , Afisa ustawi wa jamii, Serikali za mitaa na Kijiji pamoja na Mashirika ya huduma ya msaada wa Sheria.
Maadhimisho ya siku 16 za ukatili wa kijinsia huanza kuadhimishwa Kila ifikapo Novemba 25 na kilele chake huadhimishwa Disemba 10 huku yakiwa na kaulimbiu zenye jumbe mbalimbali ambapo kampeni Mwaka 2023 ni "Nyumbani kwangu hakuna ukatili", na dhamira ya kampeni hii ni kuwahamasisha wanajamii kukemea ukatili tangu Nyumbani.
0 comments:
Post a Comment