Nafasi Ya Matangazo

November 26, 2023

 




Timu ya Mpira wa miguu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeibuka na ubingwa wa mabao 4 - 2 dhidi ya Timu ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ikiwa ni kwa mikwaju ya penati kwenye mchezo wa Mpira wa miguu kwa wanaume wakati wa kilele cha mashindano ya SHIMMUTA mwaka 2023 yaliyohitimishwa leo Novemba 25 kwenye uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.

Akizungumza wakati wa kilele hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule ameelekeza Watanzania wapende kushiriki kwenye michezo kwani michezo ni afya.

"Mkoa wa Dodoma upo mstari wa mbele kwenye michezo kwani Ina vilabu 36 vilivyosajiliwa na vinafanya mashindano ya ndani. Nitoe Wito kwa Watanzania kupenda michezo kwa kucheza kila siku ya Jumamosi ya pili ya mwezi ili kuimarisha afya zenu. Serikali ya awamu ya Sita imefanya uwekezaji Mkubwa kwenye michezo na kusaidia nchi yetu kupiga hatua kitaifa na Kimataifa. 

"Pia niwapongeze sana kwa kufanya matendo ya kijamii kwani nimesikia mumetembelea vituo vya watoto yatima pamoja na wazee vya Safina, Kisebeti, Nyumba ya Matumaini, one stop centre cha Hospitali ya General n.k" Mhe. Senyamule

Akitoa neno la kufunga mashindano ya SHIMMUTA mwaka huu, Mwenyekiti wa SHIMMUTA Bi. Roselyne Massam, amewashukuru wakuu wa Mashirika, Taasisi na Kampuni kwa kuwaruhusu wafanyakazi wao kushiriki michezo kwani ni moja kati ya vipaombele vya Serikali.
Amesema mashindano haya yanawasaidia wafanyakazi kutengeneza umoja baina yao na kufahamu namna ya kusaidiana pindi wanapohitaji msaada. 

Ameongeza kuwa kazi kubwa ya SHIMMUTA ni kusimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi yanayotolewa kila wakati wanapokutana kwa ajili ya mashindano.

Naye Katibu wa SHIMMUTA Dkt. Masiatu Masinda, amesema mashindano ya mwaka huu yameshirikisha Mashirika na Taasisi 58 yakiwa na wanamichezo takribani 3,471 walioshiriki michezo zaidi ya 12. Wakiwa chini ya Mlezi wa SHIMMUTA ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, wameweza kutekeleza maagizo yake ikiwa ni pamoja na kufanya matendo ya kijamii pamoja na kutunza mazingira.

Washiriki wamefanikiwa kutembelea vituo vinne vya watoto wenye uhitaji na kuchangia vifaa vyenye thamani ya shilingi 2,255,000/= na leo ikiwa ni kilele cha mashindano haya, washiriki kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule wameshiriki jogging kwenye uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma. 

Mashindano hayo yaliyodumu kwa takribani siku 14, yameshirikisha Mashirika 57 na Michezo 12 ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa Pete, Mpira wa kikapu, Mpira wa wavu pamoja na Michezo ya jadi kama kuvuta kamba, kumkimbia, bao, n.k iliyochezwa katika viwanja mbalimbali vya Jijini Dodoma vikiwemo Jamuhuri, Chinangali, Wajenzi, Kilimani Club, kituo cha mambo poa pamoja na viwanja vilivyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM).

Washindi wa michezo hii wamekabidhiwa vikombe na medali huku vyeti vya ushiriki vikitolewa kwa Mashirika, Taasisi na Kampuni washiriki. Mashindano ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo "SHIMMUTA familia moja, familia moja, SHIMMUTA "
Posted by MROKI On Sunday, November 26, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo