Nafasi Ya Matangazo

July 28, 2023







Wizara za Kisekta zimekutana leo Julai 28,2023  jijini Dodoma kwa lengo la kujadili Mpango Kazi wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori nchini ikiwa ni mkakati maalum ndani ya Serikali wa kupunguza athari za wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa  Kikao ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Bw. Anderson Mutatembwa amesema kuwa Wizara za Kisekta zimepata uelewa wa pamoja  kuhusu Shoroba za Wanyamapori. 

"Nina imani kupitia kikao hiki tutapata uelewa wa pamoja na  itasaidia katika mipango na utekelezaji wa miradi yetu yote kwenye Wizara zote za Kisekta, moja tutakuwa tumeshafahamu shoroba ni nini na pale tunapokuwa na mashaka tukawasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii " alisema Mutatembwa. 

Amefafanua kuwa changamoto ya kuvamiwa kwa maeneo ya  Shoroba za Wanyamapori  ni suala mtambuka linalogusa Wizara mbalimbali za Kisekta akitolea mfano wa TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Amesema baadhi ya Shoroba ziko kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ambayo nayo pia yamevamiwa kutokana kutokuwepo kwa uratibu ndani ya Serikali hivyo kikao hicho kitatatua changamoto hiyo.

Amesema kuwa  kuna maeneo ya shoroba ambayo ndani yake kuna vijiji ambavyo vimesajiliwa na TAMISEMI, mengine yapo ambayo yana wawekezaji ambao wamepewa mashamba na Wizara ya Ardhi.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba amesema matarajio ya kikao hicho ni  kuboresha masuala ya uhifadhi na utalii na kwamba kila Wizara na kila Sekta ina jukumu la kufanya shughuli za uhifadhi na kuboresha masuala ya utalii kwa ujumla.

Aliongezea kuwa, baada ya maeneo ya shoroba kufanyiwa tathmini endapo yataonekana kutokuwa na sifa ya kuwa Shoroba shughuli za wananchi zitaendelea kufanyika kama kawaida.

Kwa upande wake  Mtafiti Mkuu Wanyamapori,  kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Hamza Kija  amesema  Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori iliainisha takribani Shoroba 61 nchini ambapo kati ya hizo zikachaguliwa shoroba 20 za kipaumbele  kutokana na umuhimu wake kiikolojia,kiuchumi, kisiasa, na umuhimu katika shughuli za utalii.
Posted by MROKI On Friday, July 28, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo