Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman.Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema nguvu ya pamoja kati ya Jamii, Asasi za Kiraia na Taasisi za Dini ni muhimu, ili kuiokoa Nchi kutokana na balaa la mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, huko Ofisini kwake Migombani, katika Kikao Maalum cha Asasi za Kiraia na Taasisi za Dini, kuhusu Mpango wa Urithi wa Kijani Zanzibar (Zanzibar Green Legacy).
Amesema nguvu hiyo inahitajika kutokana na ukweli kwamba, hakuna balaa linaloipata dunia kwa sasa, zaidi ya majanga yanayosababishwa na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Hapa kwetu sote ni mashahidi kwamba hali yetu ni mbaya na inazidi kuwa mbaya, na athari zimeanza kitambo licha ya kuwepo hizo juhudi zinazochukuliwa ili kuweza kukabiliana nazo”, amesema Mheshimiwa Othman.
Amebainisha kwamba athari hizo zipo kwa kiwango, daraja, na namna tofauti, zikiwemo zile za ngazi ya kidunia ambazo ni vigumu au hakuna njia ya kukabiliana nazo, mathalan mafuriko, vimbunga na matetemeko ya ardhi.
Bali, amesema, zipo athari za ndani, ambazo kwa hapa Tanzania zinabainika waziwazi, zikiwemo za ukosefu wa mvua, shida za upatikanaji wa maji, sambamba na maeneo mengi kuvamiwa na bahari, ambapo hapo kabla hali haikuwa hivyo.
Mheshimiwa Othman ameendelea kutaja athari hizo kuwa ni pamoja na upotevu unaoendelea taratibu wa Miti, Mimea na Mazao ya Matunda ya asili yakiwemo Chocha, Mbura na Pilipili-Doria; na la kusononesha zaidi ni pale ambapo kama kwamba jamii haitanabahi wala kutafakari kuchukua hatua za dharura, kunusuru hali hiyo.
Amefahamisha kuwa athari zote hizo zinasababishwa na uharibifu wa mazingira wa namna tofauti kutokana na mitazamo ya watu na namna wanavyofikiria katika harakati za maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Othman amesikitikia kwamba mapungufu hayo yanajiri wakati ambao Taifa likikabiliwa na Ongezeko kubwa la Idadi ya Watu, ambapo Takwimu zinaonyesha kuwa Mwanzoni mwa Miaka ya 2000, Zanzibar ilikuwa na Takriban Wakaazi 500,000 (Laki Tano), bali kwamujibu wa Sensa ya Mwaka 2022, wamefikia Milioni Moja na Laki Nane (1,800,000) ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba, hali ambayo inazidi kuwa tishio kwa mnasaba rasilimali, majanga na mazingira kwa ujumla.
“Sisi kama Serikali na Ofisi yetu ikiwa ndiyo yenye dhamana ya kuratibu namna ya kukabaliana na athari za kimazingira zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, tunao wajibu wa kuelekeza namna ya kujipanga; sisi inawezekana tumechelewa lakini bado hatujachelewa”, amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa licha ya udogo wa Nchi ya Zanzibar, upo uwezekano wa kufanikisha Mikakati na Mipango ya Utekelezaji kwaajili Maendeleo kupitia Mazingira, bali la msingi ni kujipanga ili kukabiliana na balaa la mabadiliko ya tabianchi.
Katika kueleza dhamira ya sasa ya Ofisi yake katika kuikabili changamoto hiyo ya ulimwengu, Mheshimiwa Othman amesema sasa ipo haja ya kutekeleza Mkakati ambao yeye binafsi kwa mashirikiano na Watendaji wake wameibuka nao, ambao unaitwa Mpango wa Urithi wa Kijani Zanzibar (Zanzibar Green Legacy).
Amebainisha kuwa, pamoja na mambo mengine, Mpango huo Mpya unalenga kurekebisha fikra ‘mindset’ za watu ambao hadi sasa hawajaelewa juu ya umuhimu wa miti na mimea kwa maisha ya mwanadamu.
“Moja ya matatizo yetu makubwa ni ‘mindset’ ambapo watu hawajaelewa kabisa na wanahitaji kuelimishwa umuhimu wa mimea maishani; hivyo ‘Green Legacy’ inakuja sasa kwa nia ya kutengeneza ili pia kurithisha kizazi kijacho Nchi yenye mazingira bora yaliyosalimika”, amefafanua Mheshimiwa Othman.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, Sheikh Abdulla Talib Abdulla amesema, kuyatunza mazingira na vyote viliomo ndani yake ni kuheshimu Uumbaji Wake Mwenyezi Mungu, hivyo kila mmoja anapaswa kuwekeza na kuungamkono juhudi katika kuepusha madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mchungaji Lydia Yesaya Mwimi, kutoka Dhehebu la Lutheran, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake na kusema Mipango na Mikakati ya namna hiyo itajenga ufanisi katika kukabiliana na athari za kimazingira zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
Viongozi na Watendaji mbali mbali wamejumuika katika Kikao hicho, wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman; na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak.
Waliohudhuria wengine miongoni mwa Viongozi na Watendaji kutoka Taasisi za Dini na Asasi za Kiraia Nchini, ni pamoja na Sunil Bhagwanji Meisuria wa Dhehebu la Hindu; Sheikh Salum Nassor Salum, Katibu wa Jumuiya ya Istiqama Zanzibar; na Bi Safia Mkubwa Abdalla kutoka Taasisi ya SAZANI.







0 comments:
Post a Comment