Nafasi Ya Matangazo

March 27, 2023

 






Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali itazitatua changamoto za ukosefu wa baadhi ya huduma muhimu kwa wananchi wa Kijiji cha Bumbwini Kiyongwe Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.

Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, ameyasema hayo leo Machi 27, huko Bumbwini-Kiyongwe mkoa wa Kaskazini Unguja, katika muendelezo wa ziara yake ya kuzitembelea familia mbali mbali kwa lengo la kuwajulia hali na kuwafariji wale waliofikwa na changamoto tofauti.
 
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa na wakaazi wa kijiji hicho ni pamoja na ukosefu wa miundombinu bora ya barabara ikiwemo kukosekana kwa gari za abiria na maji safi na salama, jambo linalowafanya wahudumu wa afya na walimu wa skuli ya Kijiji hicho ambao wanaishi nje ya hapo kuchelewa kufika katika vituo vyao vya kazi.

Awali wakaazi wa kijiji hicho walimueleza Mhe. Othman kwamba changamoto hizo zinachangia kuzorota kwa  baadhi ya huduma kwa wananchi wa huko. 

Wakaazi hao wamesema inawalazimu kutumia gharama nyingi na binafsi ili kufanikisha kuwahi katika majukumu yao ikiwemo kukodi bodaboda ama kutembea masafa marefu kwa miguu.

Kwa upande mwengine Mhe. Othman amesema viongozi kuwakaribu na wananchi kunajenga uelewa na kuweza kuona na kuyafahamu matatizo yao, sambamba na kufahamu uhalisia wa maisha ya watu jambo linalosaidia sana kujenga upendo miongoni mwao. 

Aidha, Mhe Othman, amesema kuwasikiliza wananchi na kujua changamoto zao ni nusu ya utatuzi, hivyo bado suala la kukutana na wananchi linabaki kuwa ni njia sahihi na muhimu kwa kiongozi.

Mhe. Othman kwa nyakati tofauti katika ziara yake hiyo ndani ya mkoa wa Kaskazini Unguja, amesema njia nzuri ya kumuenzi Mzee aliyetangulia ni kuyaendeleza matendo mema aliyoyaacha.
"Kiongozi wetu Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, alituachia utaratibu mzuri wa kutembeleana, kujuliana hali na kusaidiana, hivyo ni vyema nasisi kuuendeleza urithi huo mwema", amenasihi Mhe. Othman akiwataka viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama cha ACT Wazalendo kulizingatia jambo hilo. 

Kwa upande wake Katibu wa Haki za binaadamu wa Chama cha ACT Wazalendo Bi. Pavu Abdallah Juma, amesema muendelezo wa ziara hizi sio tu zinaibua changamoto za wananchi bali zinajenga matumaini ya wananchi kwa viongozi wao.

Akitoa salamu za Chama cha ACT Wazalendo za mkoa wa Kaskazini A (kichama), Mwenyekiti wa Mkoa huo Bw. Juma Khamis Juma, ameahidi mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais kushuka kwa wananchi ili kuendeleza ada hio njema kwa wananchi wao.

Masheha na Viongozi mbali mbali akiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Bw. Salim Bimani, wameambatana na Mheshimiwa Othman, katika ziara hiyo.

Ziara hiyo iliyofanyika leo katika majimbo ya Bumbwini, Donge, Tumbatu, Nungwi, Mkwajuni, Kijini, Chaani na Mahonda yote ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, itaendelea siku ya kesho Machi 28, 2023 katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Posted by MROKI On Monday, March 27, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo