WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi, hivyo ni jukumu la viongozi kuikagua na kujiridhisha kama utekelezaji wake unafanyika kwa viwango vilivyokusudiwa na unalingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa.
Ameyasema hayo jana (Jumanne, Februari 14, 2023) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Kakozi wilayani Momba akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Songwe ya kukagua miradi ya maendeleo na mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapata katika kipindi cha miaka miwili.
Akiwa katika kijiji hicho kabla ya kuzungumza na wananchi, alikagua ujenzi wa mradi wa kimkakati wa soko la Kimataifa la mazao ya kilimo na mifugo pamoja na maghala sita ambapo alisema ameridhishwa na hatua iliyofikia na kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba kwa utekelezaji wa miradi hiyo.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 8.6 unatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, pia unahusisha ujenzi wa mnada wa kuuzia mifugo, josho, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo na hivyo kuwezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Momba Condester Sichalwe alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha nyingi kupelekwa jimboni kwake katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo zikiwemo shilingi bilioni 7.8 zinazojenga miradi ya maji.
Mbali na mafanikio hayo mbunge huyo ameiomba Serikali ikamilishe usambazaji wa umeme vijijini pamoja na ujenzi wa hosteli katika shule za sekondari, ambapo Waziri Mkuu alimueleza kuwa vijiji 22 kati ya 72 vitapatiwa umeme kwani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania ikipata umeme.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika Mji wa Tunduma ambapo aliwaeleza kuwa Serikali itaendelea kuwapelekea miradi ya maendeleo kulingana na mahitaji yao, pia alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji huo kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato.
Naye, Mbunge wa Tunduma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde aliipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 kwenye jimbo hilo katika kipindi cha miaka miwili.
Aliitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa katika jimbo hilo kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa Songwe kwa gharama ya shilingi bilioni nne, ujenzi wa vituo vitano vya afya shilingi bilioni 2.5, ujenzi wa miradi ya maji shilingi bilioni nne, ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Maporomoko shilingi bilioni moja. Pia bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka shilingi bilioni moja hadi shilingi bilioni nne.
0 comments:
Post a Comment