Vitendea kazi vilivyotolewa na Shirika la MDH (Management
and Development for Health) Mkoani Tabora kwa ajili ya kusaidia watoa huduma za
afya ya jamii majumbani kufanikisha utekelezaji shugjui zao kwa weledi mkubwa.
************
Na Lucas Raphael,Tabora
SHIRIKA lisilo la kiserikali
la MDH (Management and Development for Health) Mkoani Tabora limetoa msaada wa
vitendea kazi kwa watoa huduma za afya kwa jamii (CHW) vyenye thamani ya zaidi
ya sh mil 27.
Akipokea vifaa hivyo jana
Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Kapela amelipongeza
Shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 za kuboresha
utoaji huduma za afya kwa jamii.
Alisema watoa huduma hao
wanafanya kazi nzuri sana ila wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira
magumu, hivyo msaada huo umekuja wakati mwafaka, sasa kazi iliyobaki ni
kuboreshwa huduma za afya zinazotolewa kwa jamii.
Alisisitiza kuwa vifaa hivyo
(baiskeli 8 na bajaji 3 za kisasa) vinapaswa kutumika kwa kazi iliyokusudiwa na
sio vinginevyo, kwani vimeletwa kwa lengo moja tu la kusogeza huduma za afya
karibu na walengwa.
‘Ndugu zangu mmepata vitendea
kazi, nendeni mkaboreshe huduma zenu, msitumie vifaa hivi kubeba abiria,
mkiviharibu mtakuwa mmejiharibia wenyewe, kumbukeni mlivyokuwa mnahangaika
kwenda kwa wateja’, alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa
hiyo Seif Salum alisema vifaa hivyo ni nyenzo muhimu ya kuboresha huduma za
afya kwa wagonjwa wa majumbani hasa wale wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi
(VVU) na wenye kifua kikuu (TB).
Aliomba wadau wengine
kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za
kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya ikiwemo manunuzi ya
vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa
Manispaa ya Tabora Pascal Matagi alisema basikeli 8 zimegharimu kiasi cha sh
1,920,000/- na bajaji 3 za kisasa zenye matairi 4 zimegharimu sh 25,500,000.
Aliongeza kuwa baiskeli
zitagawiwa katika zahanati za kata ya Ikomwa (Ikomwa), Misha (Itaga), Itonjanda
(Manoleo), Ndevelwa (Ndevelwa), Ipuli (St Anna), Ng’ambo (St Filipo), Tumbi
(Tumbi) na Kakola (Kakola).
Alisisitiza kuwa bajaji
zimetolewa kwa Hospitali ya Rufaa Kitete, Zahanati ya Town Clinic (Chemchem) na
Zahanati ya Cheyo, ili kuwarahisishia utoaji huduma watoa huduma za afya ya
jamii wa majumbani.
Mratibu wa Shirika la MDH, Dkt
Agness Maduka alisema wametoa vifaa hivyo ili kuboresha utoaji huduma kwa
wagonjwa walioko majumbani haswa walio na maambukizi wa TB na VVU.
Alisema ili kuwaongezea
ufanisi watoa huduma (CHW) watakuwa wanatoa mafuta ya bajaji hizo na kuzifanyia
matengenezo punde zinapoharibika, hivyo akawataka kuzitumia kwa kazi
iliyokususiwa huku akitahadharisha kuwa zimefungwa kifaa maalumu cha kuona kila
kinachofanyika.
0 comments:
Post a Comment