Benki ya CRDB imekabidhi kituo cha mawasiliano katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ikiwa ni matokeo ya fedha zilizokusanywa katika mbio za CRDB Bank Marathon 2021. Kituo hicho cha kisasa na cha kwanza kwa hospitali hapa nchini kimekabidhiwa kwa uongozi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla aliekua Mgeni Rasmi katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa maendeleo ya sekta ya afya nchini kupitia Sera ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI Policy) ambayo inaelekeza Benki kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka kwa ajili ya kutatua changamoto katika sekta ya afya, elimu, mazingira, na uwezeshaji kwa wanawake na vijana.
Katika sekta ya afya Benki ya CRDB imejikita zaidi katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na pia huduma za kibobezi (specialist services), ikiwa ni pamoja na ufadhili wa ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya, wodi za wagonjwa pamoja na utoaji wa vifaa tiba katika vituo vya afaua , zahanati na hospitali mbalimbali nchini.
“Mwaka 2020 Benki ya CRDB ilianzisha mbio za hisani zilizopewa jina la CRDB Bank Marathon kwa lengo la kusaidia jamii kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Kupitia mbio hizi mnamo mwaka 2021, tukishirikiana na washirika wetu ambao baadhi tupo nao hapa tulifanikiwa kukusanya takribani Shilingi Milioni 500 ambapo kati ya hizo tulitenga kiasi cha Shilingi Milioni 102 kufadhili ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja chini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma, elimu na ushauri juu ya Saratani kwa watanzania wengi” aliongeza Nsekela.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ocean Road, Dkt. Julius Mwaiselage ameishukuru Benki ya CRDB kwa kusaidia ujenzi wa kituo hiko cha mawasiliano ambacho kinakwenda kuisaidia katika kutekekeleza malengo ya kuanzishwa kwake hususan upande wa kuongeza uelewa wa ugonjwa wa Saratani jambo ambalo ni muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
“Tunaishukuru Benki ya CRDB sambamba na washirika wake Sanlam, Strategis na Alliance Insurance pamoja na wakimbiaji zaidi ya elfu 5 ambao kwa kushiriki kwao katika marathon ile ya mwaka 2021 leo tumeweza kuwa na kituo hiki cha kisasa ambacho kinakwenda kuokoa maisha ya Watanzania” alsema Dkt. Mwaiselage.
Makabidhiano hayo yalitanguliwa na matembezi ya hisani yalioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe, Amos Makalla yamefanyika katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Dar es Salaam yakilenga kuongeza ufahamu wa ugonjwa wa saratani.
Sehemu ya washiriki wa matembezi hayo walikua ni mashujaa waliopona ugonjwa wa Saratani ambapo walisisitiza umuhimu wa kupima saratani mara kwa mara kwani kugundulika kwa mapema kwa saratani kuna mchango mkubwa katika matibabu yake.
Akizungumza katika halfa hiyo Mhe. Makalla amesema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga fedha za kutosha kwenye sekta ya afya na kuhakikisha kunakua na mgawanyo mzuri wa vituo vya afya katika ngazi zote ili kuhakikisha wananchi kutoka maeneo yote ya nchi wanapata huduma bora za afya.
Kwa upande mwingine Mhe. Makalla aimeipongeza Benki ya CRDB na washirika wake kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hiko kama walivyoahidi wakati wakihamaisha ushiriki wa mbio za CRDB Bank Marathon na kuahidi kuwa ataendelea kuwa mshiriki wa mbio hizo kama ambavyo amefanya katika miaka miwili iliyopita.
“Mimi ni shahidi mzuri wa mbio hizi na naamini CRDB Bank Marathon ya mwaka huu itakua bora zaidi ya zilizopita na natoa wito kwa wadau kushiriki kwa wingi katika mbio hizi kwani fedha zinazopatikana katika mbio hizo zinarejeshwa kwenye jamii hususan kwenye sekta ya afya” aliongeza Mhe. Makalla.
Pamoja na ujenzi wa kituo hiko, mbio za CRDB Bank Marathon kwa mwaka 2021 ziliweza kusaidia matibabu ya watoto zaidi ya 100 wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo pia kwa mwaka jana kupitia mbio hizo jumla ya Shilingi Milioni zilipelekwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Shilingi zilipelekwa katika Hospitali ya CCBRT kusaidia wanawake ambao wana ujauzito hatarishi.
0 comments:
Post a Comment