Wakurugenzi wa bodi ya EWURA wakiongozwa na Kaimu Mha. Mkazi wa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) wakielekea kwenye jumba la kuendesha mitambo (Power House).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA Prof. Mark Mwandosya akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa ziara waliyoifanya katika mradi wa JHNPP.Kaimu Mha. Mkazi wa mradi wa JNHPP Justus Mtolera akifafanua jambo kwa Bodi hiyo walipotembelea mradi wa Bwawa la lufua Umeme la JNHPP
Meneja wa mradi wa JNHPP Mha. Said Kimbanga akifafanua jambo kwa bodi ya Wakurugenzi walipotembelea eneo la kituoa cha kupokea na kusafirisha Umeme lililopo ndani ya mradi huo.
*************
Na Mwandishi WetuBodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) linalojengwa Rufiji mkoani Pwani litaondoa changamoto za upungufu wa umeme wa uhakika kwa wananchi ambapo mradi huo unategemewa kuzalisha megawati 2115 pindi utakapokamilika mwezi Juni 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya siku moja katika mradi huu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Mark Mwandosya amesema, mradi wa JNHPP ni wa kisasa kwa sababu ni mradi mkubwa ukilinganisha na miradi mingine ambayo imeshajengwa lakini pia utazalisha umeme kwa kiwango kikubwa na utawezesha watanzania kupata umeme wa uhakika.
“Kama nilivyosema uzalishaji wa umeme utakuwa mkubwa kwa hiyo kwa miaka mingi sitegemei kwamba tutakuwa na uhaba wa upatikanaji wa umeme. Umeme ni mfumo lakini pia mambo mengine yanayoambatana na nayo ni njia za kusambaza umeme, njia za kupeleka umeme kwenye vyanzo, sasa lazima kila wakati kuwe na uhakika kwamba unapojenga njia za namna hii lazima uhakikishe mwishoni kwenye matumizi na njia zake zinakuwa imara. Kwa hiyo kwa upande wa uzalishaji tutakuwa vizuri, na lazima tuweke miundombinu vizuri kutoka kwenye njia kuu zenyewe na kuushusha umeme kwenye njia za kawaida mpaka kwenye viwanda na majumbani” amesema Prof. Mwandosya.
Ameongeza kuwa Serikali chini ya Rais mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya vizuri katika kuuendeleza mradi huu kwa kasi kubwa huku akitoa angalizo kuhusu biashara ya vyuma chakavu inayopelekea uharibifu na upotevu wa miundombinu hasa ya umeme na kuitaka Serikali iwachukulie hatua watu wote watakaohusika kufanya uharibifu wa miundombinu ya umeme hasa wafanyabiashara wa vyuma chakavu ambao ndio wanaochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa minara na nyaya na kupelekea miundombinu ya umeme kuharibika.
“Kuna suala ambalo ningependa kulizungumzia kwa sababu wote tuko nchini hapa na sasa imekuwa ni kawaida katika nchi zetu za kiafrika, kuna kitu kinaitwa vyuma chakavu, hamna adui mkubwa wa maendeleo ya umeme kama kitu kinaitwa biashara ya vyuma chakavu wale ambao wanakwenda wanaharibu minara yetu na kuchukua nyaya na kwenda kuuza kwenye viwanda vya vyuma chakavu, mwenye kiwanda lazima nae awajibike lakini pia anayesafirisha lazima nae awajibike kwa sababu huo nao ni uhujumu wa uchumi” Amesema Prof. Mwandosya.
Naye Meneja wa ujenzi wa mradi huu Mha. Said Kimbanga alipokuwa akilielezea eneo mojawapo ndani ya mradi ambapo ujenzi wa daraja la kudumu unafanyika amesema kuwa, madhumuni ya ujenzi wa daraja hili la kudumu ni kwa ajili ya matumizi ya kupitisha mizigo itakayotumika kwenye ujenzi wa jumba la mitambo (Power House) lakini pia mara baada ya kukamilika kwa mradi huu, daraja hili litatumika kama kiunganishi kati ya mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara na mikoa ya Kati na Kaskazini ya Njombe, Iringa, Morogoro Arusha.
“Daraja hili litafupisha njia kutoka mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara kuelekea mikoa ya Kati na Kaskazini ya Morogoro, Njombe, Iringa na Arusha badala ya kupita njia ya daraja la Mkapa lililopo jijini Dar es Salaam ”Alisema Mha. Kimbanga.
Kwa upande wake kaimu Mhandisi mkazi wa mradi huo Justus Mtolera ameleeza kuwa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Bwawa la JNHPP yamefikia asilimia 80.22 na kuwa kina cha maji kimefikia urefu wa mita 124.8 kutoka usawa wa bahari mpaka kufikia Jumamosi 28 Januari 2023 ikiwa ni mwezi mmoja tokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan afunge rasmi lango la kuchepusha maji ya mto Rufiji ili kuruhusu maji kuanza kujaa ndani ya Bwawa hilo.
Aliendelea kufafanua kuwa kiwango cha maji kinachohitajika kuzalisha umeme ni kina cha mita 163 hadi mita 184 kutoka usawa wa bahari na wakati maji yanaendelea kujazwa wanahakikisha kuwa kwenye mto Rufiji maji yanapita kwa ajili ya matumizi ya viumbe hai pamoja na ikolojia.
0 comments:
Post a Comment