Nafasi Ya Matangazo

November 22, 2022

Bw. Martin Mwambene, Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa wateja - TANESCO akifafanua jitihada zinazofanywa na TANESCO kuhakikisha hali ya upungufu wa umeme inaimarishwa nchini.
Namna kiwango cha maji kilivyoshuka kwenye mabwawa.
Shirika la Umeme nchini TANESCO linawataarifu wateja wake kwamba kutokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi, uwezo
 wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji umepungua kwa jumla ya megawati 155 za umeme, hii imechangiwa na mabwawa yetu ya kufua umeme ya Kihansi, Mtera, Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani kupungua uzalishaji umeme.

Vilevile, mtambo mmoja wa Kidatu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 za umeme umepata hitilafu na mitambo miwili ya Ubungo III yenye uwezo wa kuzalisha megawati 40 za umeme ipo kwenye matengenezo kinga. Na hivyo kufanya jumla ya upungufu wa umeme kwa maji na gesi kuwa kati ya megawati 245 hadi megawati 300 za umeme kutegemeana na mahitaji ya siku husika.

Tunategemea hali hii kuimarika ifikapo wiki ya kwanza ya mwezi Disemba 2022 ambapo tutarudisha jumla ya megawati 160 za umeme kwenye uzalishaji baada ya mtambo wa Kidatu wa megawati 50 na Ubungo III wa megawati 20 kutengemaa pamoja na Kinyerezi I wa megawati 80 kukamilika ufungaji wake.

Aidha, ifikapo mwishoni mwa Disemba 2022, tunategemea kupata megawati 65 kupitia Kinyerezi I megawati 45 na Ubungo III megawati 20 na kufanya jumla ya megawati 225 za umeme kurudi kwenye Gridi ya Taifa na kupunguza upungufu wa umeme kwa kiasi kikubwa.

Katika kipindi hiki kwa kuwa kazi hizi ni za matengenezo ya mitambo ya gesi pamoja na ya maji,tutaendelea kutoa taarifa ya hali ya umeme na ratiba ya upungufu wa umeme kadri inavyozidi kuimarika kupitia tovuti yetu ya www.tanesco.co.tz, kwenye magroup ya whatsapp ya wateja, magazeti na ujumbe mfupi wa maneno (SMS).

Shirika linashukuru kwa ushirikiano linaoupata kutoka kwa wateja wake katika kutafuta majawabu.

IMETOLEWA NA;
KURUGENZI YA MAWASILIANO NA UHUSIANO KWA UMMA,
TANESCO - MAKAO MAKUU.
Posted by MROKI On Tuesday, November 22, 2022 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo