Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko (katikati) kipokea zawadi ya kinyago kutoka kwa Raisi wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamale (kulia) Septemba 8, 2022 Ofisini kwake Mtaa wa Kinindo Bujumbura nchini Burundi mara baada ya mazungumzo na timu ya wawakilishi kutoka Tanzania ambao wanashiriki Tamasha la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika kuanzia Septemba 4-12 Bujumbura nchini Burundi. Kushoto ni Msanii aliyechonga kinyago hicho Bw. Mintanga.
Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya wawakilishi kutoka Tanzania ambao wanashiriki Tamasha la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika kuanzia Septemba 4-12 Bujumbura nchini Burundi.
************
Na Eleuteri Mangi - WUSM
Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko amesema Watanzania tunafursa ya kuitangaza lugha yetu ya Kiswahili katika matamasha mbalimbali duniani ili kukieneza kwa mataifa mengine.
Balozi Mhe. Dkt. Jilly amesema hayo Septemba 8, 2022 wakati akiongea na timu ya wawakilishi kutoka Tanzania Ofisini kwake Mtaa wa Kinindo Bujumbura nchini Burundi wakati wakiwa nchini humo kwenye Tamasha la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) ambalo linafanyika kuanzia Septemba 4-12 Bujumbura nchini Burundi.
“Kiswahili ni Bidhaa, tukitangaze kwa nguvu katika maonesho na matamasha yote kwa kukitengenezea mpango wa kukiuza kwa kuuza vitabu na bidha nyingine za Kiswahili.
Kwa mfano hapa Burundi tuna Hati ya Makubaliano ya kufundisha Kiswahili na Burundi kufundisha Kifaransa nchini Tanzania" amesema” Balozi Mhe. Dkt. Jilly.
Kwa upande wao Viongozi kutoka Tanzania Dkt. Emmanuel Ishengoma Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Dkt. Emmanuel Temu pamoja na Mratibu wa Tamasha la JAMAFEST ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi Leah Kihimbi wamesema Tanzania inauwakilishi mzuri kwenye Tamasha hilo ambapo takriban washiriki takriban 200.
Hati ya makubaliano ya kufundisha Kiswahili nchini Burundi na Kifaransa nchini Tanzania ilisainiwa baina ya Serikali za nchi hizi mbili mwezi Julai 2021 wakati wa ziara rasmi ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya katika Jamhuri ya Burundi wakati huo.
Tanzania imewakilishwa kwenye Tamasha la JAMAFEST na washiriki kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, taasisi zilizochini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kikundi cha ngoma cha wanafunzi kutoka shule ya msingi Mwanyahina kutoka wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, wasanii pamoja na wajasiriamali.
0 comments:
Post a Comment