Muonekano wa baadhi ya nguzo kati ya nguzo 22 zilizoinuliwa
katika mradi wa ujenzi wa daraja la JP MAGUFULI Kigongo/Busisi jijini Mwanza. Daraja
hilo litakuwa na jumla ya nguzo 67 hadi kukamilika kwake, litakuwa na urefu wa
Kilometa 3.2 na upana Mita 28.45. Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, wakitembea katika daraja la muda,
linalotumika katika shughuli za ujenzi wa daraja la JP Magufuli jijini Mwanza.
Daraja hilo litakapo kamilika litakuwa na urefu kwa Kilometa 3.2 na upana wa
Mita 28.45 Mahandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JP MAGUFULI kutoka
kampuni Yooshin Engineering Corporation, Mhandisi Abdulkarim Majuto akifafanua
jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati wakikagua mradi huo
jijini Mwanza. Imeelezwa
kuwa Daraja la JP Magufuli, linalojengwa jijini Mwanza litakalo ziunganisha
wilaya za Misungwi na Sengerema kupitia Ziwa Victoria linatarajiwa kuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati na
litakuwa la sita kwa urefu katika Bara la Afrika kwa takwimu za sasa.
Hayo yamesemwa jijini Mwanza na Joseph Haule ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi
ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board), wakati wajumbe wa Bodi hiyo wakikagua
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo.
“Kama mnavyoona Tanzania sasa tunazidi kupaa, tumeona madaraja mengine
mengi makubwa na mazuri yakichukua rekodi lakini sasa daraja hili ndilo litakalovunja
rekodi nchini, Africa Mashariki na Kati, na kwa kweli mradi huu utakapokamilika
tutajivunia sisi watanzania”
Ameyataja madaraja marefu zaidi Afrika kwa takwimu za sasa kuwa ni Daraja
la 6th October lililopo nchini Misri lenye urefu wa km 20.5, Daraja la Third Mainland
nchini Nigeria km 11.8, Daraja la Suez Canal nchini Misri km 3.9, Daraja la
Kisiwa cha Msumbiji km 3.8, pamoja na Daraja la Dona Ana nchini Msumbiji km
3.67.
“Tumeambiwa kwamba itakapofika 2024 daraja hili litakabidhiwa kwa
Serikali kama ilivyo kwenye mkataba wa ujenzi wake, licha ya changamoto za Uviko
19, maji kuongezeka, pamoja na uwepo wa miamba chini ya maji. Inafurahisha
zaidi kwamba vifaa kama nondo na simenti zinazotumika katika mradi huu zinatoka
hapa nchini” amesema Haule.
Ameongeza kuwa Bodi ya Mfuko wa Barabara imetembelea mradi wa ujenzi wa
daraja la JP Magufuli kwa kuwa Bodi ndiyo itakayokuwa na dhamana ya kuhakikisha
kwamba daraja hilo linatunzwa wakati wote na kwamba Bodi imeridhika na
teknolojia inayotumika katika ujenzi huo.
Naye Mahandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya Yooshin Engineering
Corporation, Mhandisi Abdulkarim Majuto, ameeleza kuwa kasi ya utelelezaji wa
mradi ni nzuri na kwamba hadi sasa mradi umefikia asilimia 48.9, ambapo jumla
ya nguzo 22 kati ya 67 zimeshainuliwa na tayari wameanza kulaza beam na baada ya hapo zoezi
litakalofuata ni kumwaga zege na hatimaye kuweka lami.
Akiongelea gharama za mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambrose ameiambia Bodi kuwa ujenzi
wa daraja la JP Magufuli unagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni
716.3 na kwamba unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
asilimia mia moja. Hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu, tayari Mkandarasi
ameshalipwa shilingi bilioni 223 na Mhandisi Mshauri ameshalipwa shilingi
bilioni 3.29. Aidha jumla ya shilingi bilioni 3.1 zimelipwa kama fidia kwa
jumla ya waathirika 165 waliopisha mradi huo.
Faida za
Mradi Lameck Masunga ambae ni mkazi wa eneo la Busisi wilayani Sengerema, amewaambia
waandishi wa habari kuwa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli umeleta neema kubwa
kwa wakazi wa maeneo hayo kwani watu wengi hasa vijana wameweza kupata ajira
mbali mbali katika mradi huo wenye jumla ya ajira 764 kwa wazawa, kati ya ajira
zote 820, lakini pia biashara za usafirishaji kwa kutumia bodaboda zimeimarika kwa
kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka kwenye eneo la mradi.
Kwa upande wake Esta Jumanne ambae pia ni mkazi wa Busisi, ameishukuru
Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, kwani utakapo kamilika utaondoa adha
kubwa ya kusubiria kivuko kwa ajili ya kuvuka kwenda upande wa Misungwi, ambapo
kwa sasa inawachukua zaidi ya saa moja kuvuka kwenda upande wa pili wakati kwa kutumia
daraja itakuwa ni chini ya dakika tano.
Awali,
Mhandisi Rashid Kalimbaga ambae ni Meneja Msaidizi (Ufundi), kutoka Bodi ya
Mfuko wa Barabara, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kazi ya Bodi ya Mfuko
wa Barabara ni kukusanya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zote Tanzania
bara pamoja na madaraja yake, ili kuhakikisha kuwa madaraja na barabara zote
nchini zinakuwa kwenye ubora wake kwa vipindi vyote vilivyokadiriwa.
Daraja la JP Magufuli litakapo kamilika, litaziunganisha wilaya za
Misungwi na Sengerema ambazo zimetenganishwa na Ziwa Victoria katika barabara
kuu ya Usagara kupitia Sengerema hadi Geita. Barabara hiyo pia
ni sehemu ya barabara zilizoko kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria ambayo inaanzia
Sirari mpakani na Kenya hadi Mutukula mpakani na Uganda (792.5km).
0 comments:
Post a Comment