Waziri wa Nishati Dkt.
Medard Kalemani amesema katika siku 100
za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Sekta ya
nishati imepeleka neema kwa wananchi wa maeneno mbalimbali huku akitaja kuwa takribani vijiji 400 vimefaidika na umeme
kupitia mradi maalum wa REA.
Akizungumza hivi
karibuni katika Kipindi Maalum cha Siku 100
za Rais Samia tangu aapishwe Machi 19, 2021 kilichorushwa na vituo mbalimbali vya televisheni nchini, Dkt.
Kalemani amesema kwamba Vijiji 400 vimefikishiwa umeme ndani ya siku hizo na
kufanya jumla ya vijiji 10,361 katika ya 12,268 kuwa na umeme nchini
“Tunamshukuru sana Mhe.
Rais Samia kwa kutuwezesha kufanya kazi yetu kwa wakati, katika hizi siku 100
tumepeleka umeme vijiji 400 na tumepokea maelekezo yake kwamba ndani ya miezi
18 tuwe tumekamilisha vijiji vyote vilivyobaki. Na mimi nasema miezi 18
inatutosha hivyo tunatarajia ifikapo desemba, 2022 tutakuwa tumekamilisha
kupeleka umeme kwa vijiji vyote vilivyosalia”, alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani
aliongeza kwamba kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha sh. trillion 1.24 kimetengwa
kwa ajili ya kwenda kukamilisha zoezi la kusambaza umeme kwa vijiji vilivyobaki
ambapo mpaka sasa Vijiji 10362 tayari vimefikishiwa huduma hiyo kati ya vijiji
vyote 12268 vilivyopo hapa nchini. Zoezi hilo litakapokamilika Tanzania itakuwa
nchi ya kwanza kwa nchi za Afrika katika suala la kusambaza umeme vijijini.
Dkt. Kalemani pia
alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuweka
nguvu kubwa kwenye kuendeleza sekta ya
nishati kwa ujumla wake ambapo mwaka huu wa fedha Wizara yake imepewa sh.
trillion 2.385 fedha ambayo imeongezeka kwa asilimia 8 ukilinganisha na kiasi
cha shilingi trillion 1.97 za mwaka wa fedha
uliopita.
Akizungumzia vyanzo vya
uzalishaji umeme nchini Dkt. Kalemani alisema kwamba vyanzo vikuu vya nishati
ya umeme nchini ni gesi na maji ambapo
hivi sasa asilimia 68 ya nishati hiyo inatokana na gesi na kiwango
kilichobaki kinatokana na maji. Wakati huo huo alielezea mradi mkubwa wa kufua
umeme wa maji wa Mwalimu Julius Nyerere
(JNHPP) unaogharimu kiasi cha sh. bilioni 382 unaendelea kwa kasi kwani ndani ya miezi mitatu
utekelezaji wake umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 52.
Miradi mingine ya
kuzalisha nishati nchini ambayo tayari imetengewa fedha ni mradi wa mto
Malagalasi ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 49 na kuwanufaisha wakazi wa
Kigoma, lakini pia kuna mradi wa kusindika na kuchakata gesi (LNG)
utakaogharimu Dola bilioni 30 ambapo wakazi wa Mkoa wa Lindi watanufaika na
mradi huo kwa ajira zinazotarajiwa
kufikia elfu 20.
Pindi miradi hiyo ya kuzalisha umeme itakapokamilika, uzalishaji wa umeme nchini utakuwa umefikia megawati 5000 ambapo kwa kiasi hicho Tanzania itakuwa imejitosheleza kwenye matumizi ya majumbani, viwandani pamoja na kuendeshea mradi wa treni ya kisasa ya SGR na pia itaweza kuuza umeme huo nchi jirajini.
Dkt. Kalemani anatoa rai
kwa Watanzania wote kuunganisha umeme majumbani mwao kwani gharama za huduma
hiyo sasa zimeshushwa lakini pia kuchangamkia fursa za ajira pamoja na biashara
zitakazotokana na kupatikana kwa umeme huo ili kujikomboa kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment