Nafasi Ya Matangazo

May 23, 2019

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano,Atashasta Nditiye akizungumza na wananchi wa Winyenzele Kibakwe ambapo aliwaahidi wananchi hao kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote nchini (UCSAF) utapeleka Mawasiliano eneo hilo.

  Mbunge wa Kibakwe ,George Simbachawene (Kulia)  akimkaribisha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano , Atashasta Nditiye  kuzungumza na wananchi wa Winyenzele, Kibakwe.
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (kushoto) pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano ,Atashasta Nditiye wakisikiliza risala ya wananchi wa Winyenzele wakiomba huduma ya Mawasiliano kijijini hapo.
Wazee wa Kijiji cha Winyenzele walifanya maombi ya Kimila kwa kumpa Mbunge wao Mh. George Simbachawene  kigoda na fimbo na kumuomba awadaidie wapate mawasiliano. 
****************
Na Innocent Mungy, Dodoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Atashasta Nditiye (Mb) ameutaka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini, UCSAF, kufanya tathmini ya kuwezesha wananchi wa Winyenzele katika jimbo la Kibakwe kupata mawasiliano ya uhakika.

Akizungumza na wananchi baada ya kukagua usikivu wa mawasiliano ya simu za mkononi katika kijiji cha Winyenzele, Mh. Nditiye aliwaeleza wananchi hao kuwa kwa tathmini ya haraka iliyofanywa na Mfuko wa Mawasiliano, imeonekana kuna tatizo kubwa la mawasiliano na kuahidi kuwa Serekali kupitia Mfuko wa Mawasiliano itafanya tathmini ya uhakika ili kuhakikisha eneo hilo linapata mawasiliano haraka.

“Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua wazi kuhusu suala zima la mawasiliano kwa Watanzania, nawaelekeza UCSAF waje hapa na kuhakikisha kabla ya mwezi Disemba mwaka huu wananchi hawa wanapata mawasiliano kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inavyoelekeza kuhusu mawasiliano kwa wote” alisema Mheshimiwa Nditiye.

Akizungumza katika Mkutano huo baada ya kukagua usikivu wa mawasiliano kijijini hapo, Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Mh. George Simbachawene aliiomba Serikali kupitia Wizara ua Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwasaidia wananchi hao kupata mawasiliano kwani wanapata shida sana kuwasiliana na wananchi wenzao, ndugu jamaa na marafiki.

“Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli amehamishia Makao Makuu ya Nchi Jijini Dodoma ambako ni mwendo wa saa moja na nusu kutoka hapa. Lakini wananchi hawa wanashindwa kupata hata mawasiliano kupeleka mayai ya kuku wa kienyeji, mazao mbalimbali na biashara zingine kwani hawana mawasiliano ya simu kama wenzao wanaoagizwa kwa simu oda mbalimbali na kulipwa kwa miamala ya kifedha kupitia simu za mkononi. Naomba Serikali iwawezeshe na wao waweze kuchangia jitihada za Serekali kuhamia Dodoma,” alisema Mheshimiwa Simbachawene.

Wananchi wa Winyenzele walisoma risala iliozungumzia ugumu wa mawasiliano katika eneo hilo na kumuomba mbunge wao aiombe Serikali iwasaidie wapate mawasiliano. Aidha katika kuupokea ugeni wa Mh. Naibu Waziri Nditiye aliyekuwa ziarani kikazi kukagua usikivu wa mawasiliano katika jimbo la Kibakwe, wananchi walimpokea kwa ngoma, nyimbo na maelezo ya kuonesha jinsi wanavyopata shida ya mawasiliano.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea umeme, maji na hospitali hapa Winyenzele, lakini tunaiomba Serikali ituletee mawasiliano” waliimba wanavikundi wa Kwaya ya amani na ngoma ya wazee wa kijijini hapo kwa nyakati tofauti.

Mh. Waziri aliwasihi wananchi hao kuwa wavumilivu na kuwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imesikia kilio chao na watapata mawasiliano. 

“Rais wetu mpendwa kama mnavyomjua ni mtu wa vitendo, nilipokuwa nakuja huku nilimuaga Mh. Waziri Mkuu na anawasalimia sana. Najua lazima atatoa taarifa hizi huko juu na sisi watumishi wenu, tutahakikisha tunamsaidi Rais wetu kutekeleza ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Mtapata mawasiliano” alisisitiza Mh. Nditiye.

Serikali kupitia mfuko wa Mawasiliano Nchini (UCSAF) umewezesha Zaidi ya vijiji 500 kupata minara ya mawasiliano kwa kutoa ruzuku kwa makampuni ya simu kujenga minara maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara. Katika maadhimisho ya miaka 10 ya UCSAF, Mfuko huo ulielezea kuwa takribani 94% ya nchi inapata mawasiliano na maeneo machacheyaliyobaki yatafanyiwa tathmini ili kupatiwa mawasiliano ya uhakika.
Posted by MROKI On Thursday, May 23, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo