Viongozi wa Tanzania na Misri wakati wa utiaji saini mkataba wa awali wa ujenzi wa kiwanda cha nyama kwenye ranchi ya Ruvu. Waliokaa kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa nchini (NARCO) Profesa, Philemoni Wambura na kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya NECAI ya Misri, Ahmed Hassan Mohamed. Waliosimama mwenye tai nyekundu ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina, kushoto kwake ni Balozi wa Misri nchini Abulwafa, anayefuata ni Meja Jenerali Salah Helmy Abdelmoteleb na Brigadia Jenerali Mohamed Noureldin. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega, na Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO Paulo Kimiti.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina (Mwenye koti la bluu) akiteta jambo na Balozi wa Misri nchini Abulwafa mara baada ya kutia saini mkataba wa awali wa ujenzi wa kiwanda cha nyama kwenye ranchi ya Ruvu.
****************
Na John Mapepele
Mapinduzi makubwa yanayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika udhibiti wa magonjwa, bidhaa za mifugo zinazoingia nchini kinyume cha sheria,uboreshaji wa mbali za mifugo, utoroshaji wa mifugo nje ya nchi, uzalishaji wa mifugo na uzalishaji wa malisho bora ya mifugo vimeanza kuwavutia wawekezaji wa viwanda vya nyama kuja kuwekeza na kutoa ajira kwa wanachi na kuchangia kwenye mapato ya Serikali ya awamu ya tano.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kiwanda cha nyama cha Tan choice Tanzania. Kiwanda ambacho ni kikubwa kuliko viwanda vyote Afrika Mashariki na Kati kinachojengwa Kibaha Pwani na wakati wa utiaji wa saini makubaliano awali baina ya Tanzania na Misri ujenzi wa miongoni mwa miradi mikubwa barani Afrika wa kiwanda cha uchakataji wa nyama na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na Ngozi.
Mpina amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, dunia imeshuhudia uanzishwaji wa miradi mikubwa miwili ya viwanda vya kuchakata nyama ndani ya wiki moja ambapo kumekuwa na uwekaji wa jiwe la msingi na utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote.
“Ujenzi wa kiwanda cha hiki unapeleka salamu njema kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC),SADC,IGAD na mataifa mengine ambayo inategemea mazao ya mifugo kutoka Tanzania” aliongeza Mpina
Amesema kukamilika kwa viwanda hivyo viwili kutawezasha kuchinja zaidi ya ng’ombe 3000 mbuzi na kondoo 10000 kwa siku ambapo pia itatoa ajira za kwa watanzania zaidi ya watu 6000.
“Ilani ya CCM ibala ya 8 (d) na 25(p) inatusisitiza sana sisi sote tuliopewa dhamana, kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya nyama ili kuongeza thamani na kukuza uchumi wa nchi na wadau katika mnyororo mzima wa thamani” alisisitiza Mpina kwenye hotuba yake ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye kiwanda cha Tan Choice
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha nyama cha Tan choice Tanzania Rashid Abdilah ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa miongozo na ushirikiano wa karibu ambao umewawezesha kujenga kiwanda na kufikia asilimia 85 ndani ya miezi sita na kuahidi kukamilisha kiwanda hicho na kuanza uzalishaji ifikapo agosti 2020.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji wa saini makubaliano ya awali ya kiwanda cha “Ruvu Intergrated Industry” Waziri Mpina amesema kiwanda hicho ni cha aina yake, ambapo ngombe wazima wataletwa na kupumzishwa katika eneo maalum kabla ya kuchinjwa(holding ground) hatimaye watachinjwa na mwisho kupata nyama yenye kiwango cha kimataifa(ISO) na hadhi ya kuwa na ithibati ya “halal”.
Aidha amesema kiwanda hicho kikianza kufanya kazi kitafanya kazi ya kutengeneza bidhaa nyingine za mifugo kama mikanda mikoba na viatu na chakula cha mifugo.
Amesema asilimia 1.4 ya mifugo yote duniani inapatikana Tanzania na asilimia 11 ya mifugo yote Afrika ipo Tanzania hivyo kuna uhakika wa malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vinavyoanzishwa ambapo alitoa muda usiozidi miezi mitatu kwa timu ya wataalam wa Tanzania na Misri kukamilisha mara moja na upembuzi yakinifu ili mkataba rasmi wa ubia (Joint Venture Agreement) na uendeshaji wa kiwanda uwe umesainiwa.
Aidha, Mpina aliiomba Serikali ya Misri kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya mifugo na uvuvi hususan katika uendeshaji wa shirika la Uvuvi Tanzania(TAFICO) ambalo Serikali tayari imeshalifufua, Hiifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa samaki baharini na maji baridi.
Amesema fursa za uvuvi wa ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu(EEZ) ni kubwa kwa Tanzania kuwa eneo la kilomita 223,000 unafaa kwa ajili ya uvuvi wa samaki aina ya Jodari na utalii wa majini unaojali mazingira.
Kwa upande wake Balozi wa Misri Abulwafa amesema hatua ya uwekaji wa saini hati ya makubaliano hayo ni kielelezo cha ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 baina ya nchi zote mbili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mahmoud Mgimwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno walipongeza hatua ya Wizara ambapo walisema kuwa wizara inatekeleza
Chimbuko la mradi ujenzi wa kiwanda cha Ruvu ni kutokana na mashirikiano mazuri na majadiliano baina ya Rais Dk.John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Misri Abdel Fattah El Sis yaliyofanyika Agosti 2017 na pia kufuatia kikao cha ujumbe wa Waziri wa Mifugo wa Misri Desemba 2018 na Waziri Mpina ofisini kwake jijini Dodoma.
Utiaji wa saini kwa mradi huo umefanywa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa(NARCO) Profesa Philemoni Wambura na Mwenyekiti wa Kampuni ya NECAI ya Misri, Ahmed Hassan Mohamed katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Mwanzoni mwa wiki hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli amewaagiza viongozi wote nchini kuhakikisha wanaondoa vikwazo vyote dhidi ya wawekezaji ambao wanadhamira ya dhati ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kustawisha maisha ya wananchi wakati akifunguakiwanda cha kubangua Korosho chaYalin Cashenut Company Ltd kilichopo eneo la Msijute Mtwara vijijini.
0 comments:
Post a Comment