Nafasi Ya Matangazo

April 11, 2019

 Dkt Jim Yonazi, (mwenye suti katikati) Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwenye dhamana ya Sekta ya Mawasiliano akizungumza katika hafla ya kukabidhi kompyuta 100 kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh. Anthony Mtaka (wa pili kutoka kushoto). Wengine katika Picha ni Afisa Yawala wa Mkoa wa Simiyu bw. Jumanne Sagini na kulia kabisa ni Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote Nchini Inginia Peter Ulanga. 
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh. Anthony Mtaka (wa pili kutoka kushoto) akizungumza katika hafla ya kupokea kompyuta 100 kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini. 
Dkt. Jim Yonazi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano) (aliyesimama) akizungumza na wanafunzi mbalimbali wa kidato cha sita mkoani Simiyu waliopiga kambi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa kujiandaa na mtihani wa Kidato cha sita.
Wanafunzi mbalimbali wa kidato cha sita mkoani Simiyu waliopiga kambi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa kujiandaa na mtihani wa Kidato cha sita wakisikiliza mawaidha ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi.
********
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote Nchini (Universal Communications Service Access Fund – UCSAF) umetoa kompyuta 100 kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kuendeleza TEHAMA mkoani humo.

Kompyuta hizo zimekabidhiwa na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwenye dhamana ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh. Anthony Mtaka. 

Pamoja na kompyuta hizo 100, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF) umetoa pia programu za kuzuia mashambulizi ya virusi kwenye kompyuta (antvirus) 100, printa 5 na vifaa kadhaa vya kuunganisha kompyuta hizo kwenye umeme.

Akikabidhi kompyuta hizo Dr. Yonazi aliupongeza Uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa jitihada zake katika kuhamasisha matumizi ya TEHAMA mashuleni na katika ofisi za Serikali. 

“Nikupongeze Mh. Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa kwa uongozi wenu wenye ushirikiano na mtizamo wa pamoja na jinsi timu yako nzima inavyofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Nimefurahishwa sana na ubunifu wa makambi ya wanafunzi wanaojiandaa na mitihani, jambo hili ni la kuigwa kwa wengine” alisema Dkt. Yonazi

Aidha Dr. Yonazi aliwataka wanafunzi na wote waliofaidika na kompyuta hizo kuzitumia vizuri ikiwa ni pamoja na kuzitunza. Aliwashauri kuwa wazitumie kompyuta hizo kwa matumizi ya ziada badala ya matumizi ya kawaida. “Nawataka mjipange na kuanza kuandika programu mbalimbali za kompyuta, na sio matumizi mepesi ya kawaida. Nataka baada ya muda nije kuwatembelea na kukuta mmekuwa na weledi mkubwa wa matumizi ya TEHAMA kupitia kompyuta hizi,” aliongeza Dk. Yonazi.

Akipokea kompyuta hizo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh. Anthony Mtaka aliushukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwa kutoa kompyuta hizo kwa Mkoa wa Simiyu uliokuwa na uhaba wa vifaa hivyo kwa muda mrefu. “Nikiri kuwa msaada huu ni mkubwa sana kwa Mkoa wetu, pamoja na kuwasaidia wanafunzi wetu kwenye shule mbalimbali za Mkoa wa Simiyu, tumeelekeza msaada huu pia kwa baadhi ya Ofisi za Serikali 15 ikiwa ni pamoja na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama pamoja na maeneo ambayo ni muhimu kwa mkoa wetu kuwa na vifaa hivi,”

Akitoa maelezo juu ya mgao wa kompyuta hizo, Afisa Tawala wa Mkoa wa Simiyu Bwana Jumanne Sagini amesema shule za Sekondari mkoani humo zimepewa Kompyuta 5 kila moja, na Shule ya Sekondari ya Simiyu imepata 11 kwa ajili ya kuwa na maabara ya TEHAMA ili kutoa fursa kwa shule zingine kuja kujifunza hapo.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini Eng. Peter Ulanga akizungumza katika hafla hiyo aliahidi Mfuko utaendelea kushirikiana na Uongozi wa Mkoa huo kuchagiza matumizi ya TEHAMA kwa mashule ili kupata wataalamu wa TEHAMA kutoka Mkoa wa Simiyu. Alisema Kompyuta hizo zimetolewa kufuatia ziara ya Bodi ya Mfuko ulipopita Simiyu kukagua huduma za mawasiliano ambapo Mkuu wa Mkoa aliomba msaada wa kompyuta kwa ajili ya matumizi ya shule na maeneo nyeti Mkoani humo.

Baada ya kukabidhi kompyuta hizo, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi alitembelea Shule ya Sekondari Simiyu pamoja na kukagua chumba maalumu kinachoandaliwa kuwa maabara ya TEHAMA shuleni hapo na kuahidi kuushawishi Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuendelea kusaidia jitihada za Mkoa kuendeleza matumizi ya TEHAMA.

Hali kadhalika Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt. Jim Yonazialitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa ambako wanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule mbalimbali mkoani Simiyu wamepiga kambi kujiandaa na mtihani wa kidato cha sita. Dkt. Yonazi aliwapa maneno ya faraja wanafunzi hao na kuwataka wasome na kujifunza kwa bidi kwani taifa linawasubiri kuchukua nafasi mbalimbali.




Mwisho




Caption za Picha:









Posted by MROKI On Thursday, April 11, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo