Nafasi Ya Matangazo

February 15, 2019


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kwa pamoja wamefanya ziara kwenye kijiji cha Jasini na Kituo cha kutolea huduma kwa pamoja Mpakani cha Horohoro kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya Wilayani Mkinga, Mkoani Tanga. Pamoja na Mambo mengine Naibu Mawaziri hao waliweza kujionea changamoto mbalimbali ikiwamo ukusanyaji wa mapato kituoni hapo, pamoja na kuzungumza na wanakijiji cha Jasini na Watendaji wa Kituo hicho. 

Wadau walioshiriki ziara za Naibu mawaziri hao wakisikiliza wakati Dkt. Ndumbaro (hayupo pichani) akizungumza

Sehemu nyingine ya wadau wakimsikiliza Dkt. Ndumbaro (hayupo pichani)

Mkutano ukiendelea

Wananchi wakipata huduma kwenye kituo hicho cha kutolea huduma kwa pamoja

Dkt. Ndumbaro pamoja na Dkt. Kijaji wakimsikiliza Bw. Bilali Juma, Afisa Mkemia wa kituo cha kutolea huduma kwa pamoja mpakani Horohoro

Dkt. Ndumbaro akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na wadau mbalimbali.

Kituo cha kutolea huduma kwa pamoja cha Horohoro kilihopo Mpakani mwa Tanzania na Kenya kama kinavyoonekana pichani 

Dkt. Ndumbaro akisaini kitabu cha wageni cha kijiji cha Jasini kilichopo wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga, kabla ya kuanza ziara kwenye kijiji hicho

Naibu Mawaziri pamoja na wadau mbalimbali wakiwa wamesimama kwenye moja ya jiwe ambalo linaonyesha Mpaka wa Tanzania na Kenya.

Mhe. Dkt. Ndumbaro na Mhe. Dkt. Kijaji wakiwa kwenye Nyumba iliyojengwa mpakani mwa Tanzania na Kenya. Horohoro. Mhe. Ndumbaro akiwa upande wa Kenya na Mhe. Kijaji akiwa upande wa Tanzania. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

Mhe. Dkt. Ndumbaro na Mhe. Dkt. Kijaji wakiendelea na ziara na kujionea alama za mipaka zilizopo mpakani hapo

Mhe. Dkt. Ndumbaro pamoja na Mhe. Dkt. Kijaji wakiwa kwenye moja ya alama za mpaka

Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa ziara yao kwenye kituo cha kutoa huduma kwa pamoja cha Horohoro

Mhe. Dkt. Kijaji akitizama kitambulisho cha mjasiriamali mdogo huku Dkt. Ndumbaro akishuhudia tukio hilo. Mjasiriamali huyo aliwavuti Naibu Mawaziri hao kwa mwitikio wake chanya katika kuhakikisha kila mjasiriamali nchini anapata kitambulisho cha kufanyia biashara

Mmoja wa wanakijiji akielezea changamoto wanazokabiliana nazo kijijini hapo ikiwamo upatikanaji wa elimu kwa watoto wao ambao wanalazimika kwenda kusoma Kenya na jioni kurejea Tanzania.

Wanakijiji wakiwasikiliza kwa makini Naibu Mawaziri hawapo pichani

Naibu Mawaziri hao wakizungumza na baadhi ya wananchi wa Jasini mara baada ya kumaliza ziara kijijini hapo

Waandishi wa habari wakiwa kazini

Waheshimiwa Naibu Mawaziri wakimsikiliza Mohamed Ibrahim anayesoma Darasa la nne Shule ya Vumba Kuu iliyopo Kenya. Mohamed alikuwa amerudi nyumbani kupata chakula wakati wa mapumziko mafupi kabla ya kurudi darasani.
*******************
Watendaji wa Kituo Cha Kutoa Huduma kwa Pamoja cha Horohoro kilichopo mkoani Tanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya wametakiwa kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa ya kukusanya mapato kwenye kituo hicho yanafikiwa.

Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) walipotembelea kituo hicho tarehe 10 Februari 2019.

Dkt. Ndumbaro alishangazwa na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato wa kituo hicho ambapo takwimu zimekuwa zikipungua badala ya kuongezeka kila mwaka. ‘Kwa miaka mitatu mfululizo takwimu za ukusanyaji wa mapato ya kodi katika Kituo hiki zimekuwa zikishuka badala ya kupanda, jambo ambalo si zuri kiuchumi na linakwenda kinyume kabisa na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli’; Dkt. Ndumbaro alimwambia Meneja wa TRA kituoni hapo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo mwaka wa fedha 2017/2018, makusanyo ya kodi kwenye kituo hicho ni asilimia 81 ya malengo na mwaka wa Fedha 2018/2019 inatarajiwa makusanyo yatafikia asilimia 76 ya malengo yaliyowekwa.

Mhe. Naibu Waziri aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali yanafikiwa bila kumuonea mtu ikiwemo ubunifu wa kutatua changamoto zinazokikabili kituo hicho. Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa maji ambapo yananunuliwa kwa gharama ya Shilingi milioni sita kwa mwezi. Naibu Waziri alishangazwa na uamuzi huo wa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya maji wakati kuchimba kisima hakiwezi kugharimu zaidi ya milioni 10.

Dkt. Ndumbaro pia hakuridhishwa na ubora wa jengo la kituo hicho na kubainisha kuwa ndio sababu zinazofanya kituo hicho kutozinduliwa rasmi hadi leo.

Kwa upande wake, Dkt. Kijaji alisikitishwa na utendaji usiokuwa na kiwango wa mamlaka zote zilizopo kwenye kituo hicho na kusisitiza kuwa, kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ipo chini ya himaya yake atachukua hatua zinazostahili. Moja ya maeneo yenye udhaifu katika kituo hicho ni uchukuaji wa takwimu zikiwemo za magari yanayoingia na kutoka ambapo kila mamlaka iliyopo hapo ina takwimu tofauti.

Aidha, Mhe. Kijaji alipiga marufuku kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Mkinga kwenda Wilaya ya Muheza kufuata huduma za kodi zikiwemo za kulipia kodi mbalimbali. Mhe. Naibu Waziri alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mkinga kuwatangazia wafanyabiashara wa Mkinga marufuku hiyo na kuagiza watumishi wa TRA wa Mkoa kwenda Mkinga kutoa huduma za kikodi angalau mara tatu kwa wiki.

Kuhusu ubora wa jengo hilo, Dkt. Kijaji aliagiza apatiwe nyaraka za jengo hilo ifikapo tarehe 15 Februari 2019 ili aone majukumu ya kila mmoja katika ujenzi wa jengo hilo kwa madhumuni ya kuchukua hatua stahiki.
Mhe. Dkt. Ndumbaro na Mhe. Dkt. Kijaji walifanya ziara ya pamoja kwenye kituo hicho cha Horohoro kwa lengo la kujionea changamoto ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Posted by MROKI On Friday, February 15, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo