Na John Mapepele, Dodoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa, Luhaga Mpina
ametoa onyo kali kwa viongozi wa Serikali katika Halmashauri zote nchini
wanayoihujumu operesheni maalum ya kitaifa ya kupiga chapa mifugo inayoendelea nchi nzima kwa kutoa
taarifa za uongo zinazoonesha kuwa mifugo mingi imepigwa chapa tofauti na hali
halisi.
Mpina amesema Wizara
yake itapita kila Wilaya kufanya tathmini ya kina baada ya tarehe ya mwisho ya upigaji chapa
kitaifa iliyotolewa na Waziri Mkuu, Marchi 31 mwaka huu ambapo watendaji watakaobainika
kudanganya sheria zitachukua mkondo wake.
Aidha ametoa maelekezo
kwa Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kote nchini kuhakikisha kwamba mifugo yote
inatakiwa iwe imepigwa chapa hadi tarehe ya mwisho iliyopangwa na kusiwe na
visingizio vyaaina yoyote ikiwa ni
utekelezazi wa Sheria ya Utambuzi,Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo Namba 12 ya Mwaka 2010 na kanuni
zake za mwaka 2011.
Maelekezo hayo aliyatoa jana akiwa Naibu Waziri wake Mhe.
Abdalah Ulega na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipotembelea mnada wa
upili wa Kizota pembeni kidogo wa mji wa Dodoma kutoa tathmini ya zoezi la
upigaji chapa nchini kabla ya siku ya mwisho
ya upigaji chapa mifugo yote nchini ambayo ni tarehe 31/3/2018.
Waziri Mpina alisema,
kulingana na takwimu ambazo Wizara
imeletewa hadi Machi 11, 2018 inaonyesha
kwamba, jumla ya ng’ombe 16,744,355
kati ya 17,390,090 sawa na asilimia 96.3 ya ng’ombe wote nchini wamepigwa
chapa. Aidha, jumla ya Punda 51,494 wamepigwa chapa nchini.
“Hivi karibuni nilitembelea mnada wa Pugu nikaangalia idadi ya mifugo
iliyopigwa chapa hawafiki hata asilimia tano, lakini leo hapa sote tumeshuhudia
idadi ya mifugo wote waliopigwa chapa katika mnada huu wa Kizota ni chini ya
asilimia mbili.
Minada hii ndiyo mikubwa nchini ukianzia wa Pugu na huu ni wa Kizota ni
wa pili kwa hiyo inadhihirisha kwa uhakika kabisa kuwa kuna udanganyifu mkubwa
unaofanywa na watendaji wasio waaminifu wanaopotosha taarifa.” Alisistiza Mpina
Alisema wilaya nyingine zimeleta takwimu ambazo zinaonyesha zimepia
chapa mifugo kwa zaidi ya asilimia elfu moja ambapo amezionya kutojiingiza
katika matatizo kwa kuendelea kudanganya.
Aidha alisema tathmini ya jumla kuanzia mwezi Disemba 2017 hadi tarehe 11
Marchi, 2018 inaonyesha kwamba, Halmashauri 85 zimepiga chapa kwa asilimia 100 na
zaidi; Halmashauri 86 zimepiga chapa kati ya asilimia 50 na 100, na Halmashauri
4 zimepiga chapa chini ya asilimia 50.
Alizitaja Halmashauri hizo kuwa ni Kasulu, Madaba, Arusha na Meru,
ambapo alisema Halmashauri zilizobaki ni
miongoni mwa Halmashauri zenye ng’ombe wengi wa maziwa nchini wanaotarajiwa
kuvishwa hereni. Halmashauri hizo ni Manispaa ya Ubungo, Temeke, Moshi,
Kinondoni na Ilala.
Alisema Halmashauri zingine zenye ng’ombe wengi wa maziwa kuliko
wanaochungwa ni Rungwe, Busokelo na Kibaha.
Alisema tathmini ya zoezi la chapa tangu kuongezwa kwa muda kutoka
tarehe 31 Januari, 2018 hadi sasa inaonyesha ongezeko la Halmashauri 14 zilizopiga
chapa mifugo zaidi ya asilimia 100 na kupungua kwa Halmashauri 8 zilizopiga
chapa kati ya asilimia 50 – 100 na kupungua kwa Halmashauri 25 zilizopiga chapa
chini ya asilimia 50.
“Napenda kutoa maelekezo kwa
wafugaji kwamba mifugo yote ipigwe chapa popote ilipo ilimradi ni ya Tanzania ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima baada ya tarehe ya mwisho iliyopangwa na
Serikali ambayo ni mwisho wa mwezi huu na
ninaomba ieleweke kuwa visingizio vyoyote havitakubalika’ Alisisitiza Waziri Mpina.
Akielezea umuhimu wa zoezi hilo, Mpina alisema kwamba kukamilika kwa
zoezi hilo kutasaidia kutambua mifugo yote iliyopo nchini ili kukidhi
mahitaji ya biashara katika masoko ya
ndani na nje ya nchi,kudhibiti magonjwa
ya mifugo na kudhibiti wizi wa mifugo na usafirishaji holela.
Aidha kutasaidia kuepusha migogoro inayoendelea maeneo mbalimbaili
nchini baina ya wafugaji,wakulima pamoja
na watumiaji wengine wa raslimali ardhi na kutawezesha Serikali kupata idadi
sahihi ya mifugo iliyonayo ili kupanga kupanga mipango inayotekelezeka na kuleta mapinduzi katika sekta hiyo.
Alisema Zoezi la upigaji chapa
ni endelevu kwa mifugo ambapo alisema ng’ombe na punda wanaotimiza miezi sita wanatakiwa kupiga chapa.
Awamu ya kwanza ya zoezi la upigaji chapa ng’ombe na punda nchini
ilianza rasmi tarehe 14 Desemba, 2016 kufuatia Agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu
na ilitarajiwa kukamilika tarehe Desemba 31, 2017. Tathmini iliyofanywa baada ya kukamilika
awamu hiyo ya Desember, 2017 ilionyesha jumla ya ng’ombe 7,401,661 sawa na
asilimia 38.5 ya lengo walikuwa wamepigwa chapa.
Kutokana na kiwango kidogo cha ng’ombe waliokuwa wamepigwa chapa wakati
huo, Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Luhaga Mpina aliongeza muda wa kukamilisha
zoezi hili hadi tarehe 31 Januari, 2018. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2018
jumla ya ng’ombe 15,192,565 sawa na asilimia 87.4 walikuwa wamepigwa chapa.
Aidha jumla ya punda 6,944 walikuwa wamepigwa chapa kati ya punda 572,353
wanaotarajiwa kupigwa chapa nchini. Pia, jumla ya ng’ombe wa maziwa 58,214
walikuwa wamevishwa hereni kati ya ng’ombe wa maziwa 782,995 wanaotarajiwa
kuvishwa hereni. Pamoja na muda huo kuongezwa, Halmashauri nyingi zilikuwa bado
hazijakamilisha zoezi hili kikamilifu. Kutokana na mapungufu mbalimbali
yaliyojitokeza, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa Majaliwa alilazimika kuongeza muda
zaidi mpaka tarehe 28 Machi, 2018 na kuziagiza Mamlaka ya Serikali za Mitaa
kusimamia zoezi hili kikamilifu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kumpa taarifa ya Utekelezaji ifikapo Machi 31, mwaka
huu.
Wakati huo huo, Waziri Mpina alisema kuwa Wizara itafanya mageuzi makubwa ya kupanua
kiwanda cha machinjio ya nyama cha
Dodoma(TMC) ili kiweze kukidhi mahitaji ya sasa
ya mifugo ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa ya mifugo nchini.
Mmoja wa wafanyabiashara wa mifugo Shabani zuberi, alimweleza Waziri kuwa
kwa sasa gharama ya uchinjaji wa
nyama katika machinjio ya kiwanda hicho ni juu ukilinganisha na machinjio
nyingine nchini ambapo ni shilingi elfu ishirini kwa ng’ombe mmoja na kwamba
nyama kwa ajili ya soko la ndani inanyimwa sehemu ya kugandishia tofauti
na nyama inayosafirishwa kwenda nje ya nchi suala ambalo linawafanya
wapate hasara kubwa nyama ikishindwa kuuzika katika siku husika
kutokana na kukosa sehemu ya kugandishia.
Akijibu hoja hizo, Mpina aliielekeza menejimenti ya kiwanda hicho kukaa
na Wizara na kuangalia namna bora ya kuweka gharama ya uchinjaji itakayoendana
na hali halisi ya bei la soko.
Aidha alikiagiza kiwanda kuanza mara moja kutoa huduma ya kugandisha na
kuhifadhi nyama ya walaji wa ndani
ambapo pia alitoa wiki mbili kuhakikisha huduma ya maji inaletwa na kiwanda
hicho katika machinjio ya Kizota.Alisisitiza kuwa Mnada wa Kizota utaboreshwa
na Serikali kwa kuwa unaingiza milioni 624 kwa mwaka hivyo ukiboreshwa miundo mbinu yake
utaongeza mapato yake.
“Hatuwezi kuwajali watu kutoka nje ya nchi na usiwajali wananchi wako
wa ndani ya nchi, naamuru kwamba TMC wapeni huduma ya kugandisha nyama wateja wenu wa soko la ndani”
alisistiza Mpina.
Alimpongeza Naibu Waziri, Abdalah Ulega kwa juhudi anazozifanya za kuhakikisha minada yote nchi inakuwa na
miundombinu bora ambapo awali Mhe. Ulega alitembelea mnada wa Kizota na kujadiliana na wadau wa mnada huo
kuhusiana na mambo mbalimbali.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Selina Lyimo alimshukuru Waziri Mpina kwa maelekezo
aliyoyatoa kwa Wizara na kumhakikishia kwamba yatatekelezwa mara moja ili
kuleta mageuzi na mapinduzi makubw a
katika sekta.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti Mafunzo na Ugani,Angelo
Mwilawa amesema Idara yake itaendelea
kuratibu tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo hususan kwenye eneo
la malisho na uzalishaji wa mbegu bora za mifugo ili wafugaji waweze kufuga
kisasa
0 comments:
Post a Comment