Nafasi Ya Matangazo

June 07, 2017



 Waziri  Mkuu  Kassim  Majaliwa  akiangalia Mtoto wa Darasa la asaba Uhuru  Mchanganyiko Mariana  Alex  Mwenye  ulemavu  wa macho  , anavyo weza kuandika  kwakutumia  mashine  maalumu  ya kuandika  , June 6 2017 Waziri  Mkuu  alikabidhi  vifaa  vya Kujifunzia   katika shule mbali mbali hapa Nchini Shughuli hiyo imefanyika  Jijini  Dar es salaam
 Waziri  Mkuu  Kassim  Majaliwa  akijaribu  kuandika  kwakutumia  kifaa maalumu  chakujifunzia  kuandika  watoto wenyeulemavu  wa  Macho  6 june2017, Kulia kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Elimu na Sayansi  Profesa  Joyce  Ndalichako,  Waziri  Mkuu  alikabidhi  vifaa  vya Kujifunzia   katika shule mbali mbali hapa Nchini Shughuli hiyo imefanyika  Jijini  Dar es salaam
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi wote nchini ambao wana watoto wenye ulemavu wasiwafiche na badala yake wahakikishe wanapata elimu na kutimiza ndoto zao.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumanne, Juni 6, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, walimu na wanafunzi kwenye uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya elimu maalum uliofanyika kwenye viwanja vya ya msingi Uhuru Mchanganyiko, jijini Dar es Salaam.

“Nikiwa mwalimu kitaaluma, natambua kwamba mapungufu ya kimwili, kisaikolojia, kiakili au ulemavu wa aina yoyote si kikwazo cha kutimiza ndoto za watoto wetu. Hili linadhihirika kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema na kutoa mfano wa utumishi Serikalini ambako kuna viongozi wenye mahitaji maalum, lakini wamekuwa wakitoa mchango mkubwa bila kujali hali yao kimwili au vinginevyo.

“Hivyo, nawasihi wazazi wenzangu, msikatishe ndoto za watoto wenu wenye mahitaji maalum kwa kuwaficha. Wapelekeni shuleni wakapate elimu, iwafae maishani,” alisema.

Waziri Mkuu alisema usambazaji wa vifaa hivyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata huduma hiyo bila kujali hali yake ya kimwili, kiakili, kiafya na uwezo wa kifedha.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene ahakikishe anandaa utaratibu wa kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupangiwa bajeti kulingana na mahitaji yatakayoainishwa.

“Tunapoendelea na jitihada hizi za kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu, ni vizuri tukawa na utaratibu endelevu wa kubaini idadi kamili ya watoto hao kupitia uandikishaji wa watoto shuleni. Bila kubaini idadi yao, itatuwia vigumu kupanga bajeti kwa ajili ya watoto wetu hao. Zoezi hili linaweza kufanyika wakati wa uandikishaji na likawa endelevu kadiri wanavyopanda vidato,” alisema.

Waziri Mkuu alisema mbali ya vifaa vya wanafunzi wasioona na wenye baki ya usikivu (hard of hearing), Serikali pia imenunua vifaa kwa ajili ya walimu wao ili vitumike kufundishia na kupimia ili kubaini mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa watoto wanaoandikishwa shuleni.

Alisema vifaa vinavyoanza kusambazwa, vitasaidia kuinua kiwango cha taaluma kwenye shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum na pia vitasaidia watoto wengi zaidi wenye mahitaji maalum wapate elimu na kuongeza hamasa kwa walimu wanaofundisha kwenye shule husika.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia hadhira hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa utahusisha mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwamba zoezi hilo litazinufaisha shule za msingi 213 kati ya 408; na shule za sekondari 22 kati ya 43 zenye wanafunzi wa mahitaji maalum.

Alisema vifaa vilivyonunuliwa vimegharimu sh. bilioni 3.6 kutokana na michango ya washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (DfID) na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (SIDA) na kwamba wizara hiyo itaendelea kununua vifaa zaidi kulingana na bajeti inayotolewa.

Alivitaja vifaa vilivyoninunuliwa kuwa ni mashine za nukta nundu 932; vivunge vya kufundishia wasioona 1,495; karatasi za kuandikia nukta nundu (ream) 2,548; karatasi za kurudufishia (ream) 1,150; shime sikio (hearing aid) 1,150 na vivunge vya upimaji wa mahitaji maalum ya kielimu 78.

Naye Mratibu wa Elimu kutoka SIDA, Bi. Helena Reutersward akitoa salamu kwa niaba ya washirika wa maendeleo alisema wao wamedhamiria kuboresha sekta ya elimu hapa nchini na hasa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.

“Elimu ni muhimu ni kwa kila mtu lakini ni muhimu zaidi kwa watu wenye mahitaji maalum. Washirika wa maendeleo tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kuchangia jitihada zake za kuboresha elimu nchini Tanzania,” alisema.
Posted by MROKI On Wednesday, June 07, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo