Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Women Tears Limited, Doreen Kimbi,akimsaidia mmoja wa bibi waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
Wazee kutoa maeneo
mbalimbali ya Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro wakiwa wamejitokeza Kijiji cha Shinga, Kata ya Uru Kusini kwaajili ya
kufanyiwa uchunguzi wa afya zao chini ya Taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Tears Limited ya mjini humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Women Tears Limited, Doreen Kimbi, akizungumza baadhi ya wazee waliojitokeza kupata huduma ya uchunguzi wa afya zao.
Madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakiwafanyia uchunguzi wazee mbalimbali waliojitokeza.
****************
Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAZEE wasiojiweza 219
kutoa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro
wamepatiwa huduma ya uchunguzi wa afya zao kupitia Taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Tears Limited ya mjini humo.
Uchunguzi huo wa afya ulifanywa na timu ya madaktari kutoka
Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo walibaini maradhi mbalimbali kwa wazee hao
ikiwepo saratani ya tezi dume, kisukari na magonjwa ya moyo.
Mbali na kuwafanyia uchunguzi huo wa afya Taasisi hiyo ya
Women Tears ilisema itafanya jitihada za kuwapatia matibabu wazee hao kwa
kuwakatia Bima za Afya ya jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Doreen Kimbi alisema
juzi madaktari hao waligundua magonjwa hayo kwa wazee, baada ya
kujitokeza kupima afya bure katika Kijiji cha Shinga, Kata ya Uru Kusini, Moshi
Vijijini.
“Changamoto ni idadi kubwa ya wazee kushindwa kufikia
huduma za matibabu na kumudu gharama, na kwa kuwa mpango huu ni endelevu, sisi
kama taasisi tumeamua kutoa huduma ya uchunguzi bure, lakini hata hivyo tunafikiria
baadae kuwaunganisha katika huduma ya bima ya afya ili waweze kupata matibabu
ya maradhi yanayowasibu,”alisema Doreen.
Taasisi hiyo inajishughulisha na vita dhidi ya mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) na kusaidia wazee wasiojiweza katika
kupata mahitaji yao muhimu yakiwepo ya huduma ya afya.
Aidha, Doreen alisema taasisi yake inaunga mkono juhudi za serikali
za kutoa huduma za afya pamoja na taasisi nyingine mbalimbali ingawa bado
inaonekana kuwa changamoto ya kuwafikia wazee wote hasa maeneo ya vijijini bado
ni tatizo.
Doreen alisema ipo haja ya serikali kuifanyia kazi kwa
haraka sera ya Taifa ya wazee ambayo ilikwama kwa zaidi ya miaka kumi sasa bila
ya kutungwa na kuwa sheria ambayo ingefanya kazi na kuwasaidia wazee.
Sera ya taifa ya wazee ya mwaka 1999 pamoja na mambo
mengine imezingatia azimio la Umoja wa Mataifa namba 46 la mwaka 1991 kuhusu
haki za wazee.
“Ikiwa kama sera ya wazee ingetungiwa sheria na ikaanza
kutumika, haya ya wazee kukosa vitambulisho vya bima ya afya, matukio ya
ukatili na kutojumuishwa katika ajenda ya maendeleo tusingeyasikia mara kwa
mara. Ndio maana tunaiomba serikali ipeleke Bungeni muswada huo ili kundi hili
lijiondoe kwenye changamoto za afya na kuweza kunufaika na mipango endelevu ya
kitaifa,”alisema Doreen.
Alisisitiza ni vyema serikali ikajielekeza katika kumaliza
malalamiko ya huduma duni za afya kwa wazee ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa
baadhi ya mahitaji muhimu ya kibinadamu katika makazi ya wazee.
Aidha kupitia taasisi hiyo ya Women Tears aliomba wadau na
taasisi nyingine mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuunga mkono jitihada
hizo alizozianzisha ilikuweza kuwafikia wazee wengi na kuwapatia huduma za
matibabu.
0 comments:
Post a Comment