Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa
Waasisi wa Taifa na Waziri Mstaafu, Sir George Kahama kufuatia kifo cha kiongozi
huyo kilichotokea leo tarehe 12 Machi, 2017.
Sir George Kahama amefariki dunia akiwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika Salamu zake Rais Magufuli amesema
Taifa limempoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru,
maendeleo na ustawi wa jamii ya watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za
uongozi hususani kuwa miongoni mwa Mawaziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri
ambapo alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.
“Sir George Kahama alikuwa kiongozi shupavu,
mzalendo, mwanasiasa mahiri, aliyewapenda Watanzania na aliyejitoa kushirikiana
na viongozi wenzake akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere
kupigania uhuru, kujenga misingi ya Taifa likiwemo Azimio la Arusha, kujenga
misingi ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na mengine mengi, kwa hakika
hatutamsahau”
“Japo kuwa Sir. George Kahama ametangulia mbele
za haki, sisi viongozi tuliopo tutamuenzi kwa kuhakikisha tunaendeleza juhudi
za kuipigania Tanzania aliyoshiriki kuijenga, na pia tunamuombea kwa Mwenyezi
Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais
Magufuli katika salamu hizo.
Pamoja na familia ya Marehemu Sir. George Kahama,
Mhe. Dkt. Magufuli amewapa pole nyingi wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Wabunge, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huo.
0 comments:
Post a Comment