Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga wakati Katibu Mkuu huyo aliposimama kwa muda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,Bi. Mindi Kasiga naye akiagana na Mhe. Guterres
Mhe. Guterres akiagana na Dkt. Mahiga mara baada ya kumaliza kufanya mazungumzo yao.
***************
Na Mroki Mroki
KATIBU Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN), Antonio Guterres ameisifu Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake
za kutafuta amani nchini Burundi.
Guterres alitoa
pongezi hizo wakati aliposimama kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam akitokea nchini Kenya.
Katibu Mkuu huyo mpya
wa UN alisimama kwa ajili ya kufanya mazunguzmo na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga.
Pamoja na mambo
mengine Guterres alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa serikali kwa juhudi zake
za kutafuta amani nchini Burundi kupitia kwa Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais
mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Tanzania imekuwa
kinara wa amani Afrika na duniani na naipongeza kwa dhati katika jitihada zake
inazozifanya za kutafuta amani ya Burundi na katika nchi nyinge za ukanda huu,”
alisema Guterres.
Aidha alisema
anatambua mzigo mkubwa inaoupata kama nchi kutokana na kuendelea kupokea
wakimbizi kutoka nchini Burundi, na kuahidi UN kuendelea kuunga mkono jitihada
za kutafuta suluhu ya kisiasa nchini humo.
Kwa upande
wake; Balozi Mahiga aliwasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais John
Magufuli kuhusiana na hatua iliyofikiwa ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi na
ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya ulinzi wa amani
Mashariki wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Balozi Mahiga pia
alisema kama nchi wamefurahishwa na ujio wake na Rais amempa mwaliko rasmi wa
kufanya ziara nchini.
Aidha alimweleza kuwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),
katika mkutano wao ujao wana mpango wa kuwasilisha hoja maalum kuhusu hali ya kisiasa
nchini DRC.
Mbali na kufanya
ziara nchini Kenya, Katibu Mkuu huyo wa UN alitembelea nchi ya Somalia na
kukutana na Rais mpya wa nchi hiyo, Mohamed Abdullahi Mohamed, ambapo
aliagiza Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua kuepusha balaa la njaa nchini
Somalia, kutokana na hali mbaya ya ukame.
0 comments:
Post a Comment