Nafasi Ya Matangazo

December 03, 2016



Shule ya Sekondari Loyola imeibuka mshindi wa mashindano ya vilabu vya kodi mwaka 2016 na kujinyakulia zawadi ya Televisheni ya Inchi 40, Kompyuta ya mezani pamoja na Printa moja baada kuonesha uwezo wa hali ya juu katika kujibu maswali ya kodi wakati wa mashindano ya vilabu vya kodi yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam.

Nafasi ya pili katika mashindano hayo imeshikwa na shule ya Sekondari Kibaha ambayo ilizawadiwa Kompyuta ya mezani na Printa wakati shule ya Sekondari ya St. Joseph imekuwa mshindi wa tatu na kupatiwa Kompyuta ya mezani.

Zawadi ya shule iliyowasilisha mada bora ya kodi ilinyakuliwa na shule ya Sekondari Shaaban Robert ambapo mwanafunzi Adamson Nsimba kutoka shule ya Sekondari St. Joseph ameibuka mwanafunzi bora na kuzawadiwa  Kompyuta mpakato.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalizishirikisha shule za sekondari 47 kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kupima uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa wanafunzi ikiwa ni mkakati wa kujenga uzalendo na uhiari wa kulipa kodi kupitia shule za sekondari kwa kuwajengea uwezo wa kuwa walipakodi wa baadae.

Kati ya shule hizo zilizoshiriki, jumla ya shule 18 zilishindana katika kuwasilisha mada mbalimbali za kodi  baada ya kuibuka washindi katika mashindano ya awali yaliyofanyika Tarehe 26 Novemba 2016 katika Chuo cha Kodi (ITA) ambayo yalishirikisha shule 46 za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

 Mada ambazo ziliwasilishwa na kushindanishwa katika shindano hilo ni pamoja na  Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFD’s) na Utunzaji wa Kumbukumbu za Biashara; Uingizaji wa Bidhaa Nchini na Uuzaji wa Bidhaa Nje ya nchi; Mifumo ya Ulipaji Kodi na Kodi ya Mapato Yatokanayo na Ajira (PAYE).

Mada nyingine zilizowasiliswa katika mashindano hayo ni Uboreshaji wa Mifumo na Utawala wa Kodi Tanzania, Kodi ya Mapato Yatokanayo na Rasilimali na Mapato yatokanayo na Biashara.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Bw. Richard Kayombo alisema, mashindano hayo ya vilabu vya kodi kwa shule za Sekondari yalianza kufanyika baada ya kuzinduliwa vilabu vya kodi katika shule za Sekondari mwaka 2008 ili kukuza uelewa wa masuala ya kodi kwa wanafunzi na kuongeza hamasa ya ushiriki wa mashindano hayo. 

“Tayari TRA imezindua jumla ya vilabu vya kodi katika shule za Sekondari 220 za Tanzania Bara na Visiwani zikiwa na wananfunzi wanachama 16,620”. Alisema Bw. Kayombo

Bw. Kayombo amesema TRA itaendelea kusaidia vilabu vya kodi kadri inavyoweza kwani kupitia vilabu vya kodi Taifa linapata vijana wenye uelewa wa kodi ambao wanakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi na hivyo kupata taifa lenye uelewa wa masuala ya kodi na kujijengea utamaduni wa kulipa kodi.

Kwa upande wake Mratibu wa vilabu vya kodi Tanzania ambaye ni Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi TRA Bi. Honesta Ndunguru alisema pamoja na kuzindua vilabu vya kodi katika shule za sekondari; TRA pia imepanua wigo wa vilabu hivyo kwa kuanzisha Jumuiya za Kodi kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambao kwa pamoja na shule za Sekondari watakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi mashuleni, vyuoni na katika jamii kwa ujumla.

Mwanafunzi bora Adamson Nsimba ametoa wito kwa wanafunzi wote kujiunga na vilabu vya kodi ili wapate uelewa wa masuala ya kodi na hivyo kujijengea utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari.
Posted by MROKI On Saturday, December 03, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo