Baadhi ya maafisa wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa katika picha ya pamoja wakati wa kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini lililobeba kauli mbiu ya "Wajibu wa vijana katika uchumi na maendeleo ya jamii" kuelekea maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Mataifa lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kufanyika jana jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
****************
Kufuatia
changamoto ya uhaba wa ajira hususani kwa vijana nchini, wametakiwa
kuwa wabunifu na watafutaji wa fursa za kujiajiri badala ya kuilalamikia
serikali kuwa haitatui changamoto hiyo kwa muda mrefu.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na
Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza katika Kongamano
la Vijana lililobeba kauli mbiu ya "Wajibu wa vijana katika uchumi na
maendeleo ya jamii" lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kufanyika
jana jijini Dar es Salaam kuelekea sherehe za maadhimisho ya wiki ya
Umoja Mataifa, amesema vijana inabidi wawajibike katika kuleta maendeleo
ya uchumi kwenye jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla.
Pia
amesema vijana waache kuhoji serikali kuwa inawafanyia nini badala yake
wawe wazalendo kwa kuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya Taifa lao.
"Tuna
kazi kubwa ya kujenga fikra za vijana kwamba ili kufanikiwa katika
maisha siyo lazima kuajiriwa, vijana wengi ukiwahoji wanakwambia
changamoto kubwa wanayoikabili ni ukosefu wa ajira. Lakini wanasahau
kuwa changamoto zipo nyingi zinazowakabili," amesema.
Prof.
Ole Gabriel amezitaja changamoto nne zinazokabili vijana ambazo
zinasababisha washindwe kujiajiri au kushindwa kujiendeleza pindi
wanapojiajiri kuwa ni, ukosefu wa fikra kutokana kwamba wengi
hawaziruhusu fikra zao kubuni mbinu za kujiajiri. Changamoto nyingine
aliyoitaja ni vijana kukosa uelewa, mbinu na ubunifu wa kuongeza thamani
ya shughuli wanazofanya.
Changamoto
nyingine aliyoitaja ni mfumo mbovu na usio rafiki kwa vijana hasa
mifumo duni ya upatikanaji mitaji na masoko, hususani katika kipindi
hiki ambacho kuna wimbi kubwa la vijana wasio na ajira.
Ameshauri
kuwa "Hivi sasa kuna elimu ya ujasiriamali lakini niseme tu
haitomsaidia kijana kujikwamua sababu hutoa elimu ya uzalishaji pekee.
Ili kijana afanikiwe na ujasiriamali, kwanza inabidi apewe elimu ya
kufanya utafiti wa bidhaa inayohitajika kwa kipindi husika, akishajua
bidhaa hitajika ndipo afanye uzalishaji kisha hatua ya mwisho kutafuta
masoko ambayo tayari ameshayafanyia uchunguzi."
Pia
ameshauri vijana kuwekeza katika biashara kilimo kwa kuwa ndiyo sekta
pekee yenye fursa ya kutoa ajira kwa wingi kwa kuwa imeajiri asilimia 84
ya vijana.
"Tanzania
ina vijana zaidi ya milioni 16.2 ni sawa na asilimia 70 ya watanzania,
waliofanikiwa kuajiriwa katika sekta binafsi ni milioni 1, waliojiajiri
milioni 1.1 waliopo katika sekta ya umma ni 18,8000 na katika sekta ya
kilimo wapo vijana milioni 13.2 na bado nafasi zipo katika sekta hiyo,"
amesema.
Hata
hivyo, Prof. Gabriel amewaasa vijana kutotumia utandawazi vibaya hasa
mitandao ya kijamii kutokana kwamba imekuwa sababu ya vijana wengi
kutokuwa na maadili.
"Utandawazi
unabomoa uwezo wenu wa kufikiri, zamani vijana walikuwa wanakimbilia
kuwekeza katika sekta ya kilimo ila sasa kutokana na utandawazi
wanakimbilia kutafuta ajira hata kama fursa hakuna," amesema na
kuongeza.
"Msipoangalia
miaka michache ijayo tutakuwa watu wa teknolojia na mitandao. Maadili
mema tuliyojengewa yatapotea kwa sababu ya kufikiri kwamba mitindo ya
kimaisha kutoka nje ndiyo inafaa kuliko ya kwetu, inabidi turudishe yale
maadili ya zamani sababu nchi yoyote isiyokuwa na maadili, tamaduni
imeparanganyika na haina maendeleo," amesema.
Mwakilishi
kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Annamarie Kiaga akizungumza kwa
niaba ya UN amesema kuwa shirika hilo litahakikisha linawezesha vijana
kushiriki katika maendeleo ya uchumi kwa kuwainua kiuchumi pamoja na
kutoa elimu ya namna ya kujiajiri.




0 comments:
Post a Comment