Nafasi Ya Matangazo

September 23, 2016

Displaying DSC_7362.JPG
Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill, Salehe Beleko (kulia) akionesha sehemu ya madawati 4,112 yanayotengenezwa na shamba hilo kwa ajili kuunga Mkono Mpango wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha Shule zote nchini zinakuwa na madawati ya kutosha. Wengine pichani ni watendaji katika shamba hilo.
Displaying DSC_7399.JPG
Moja ya kitalu cha miche ya miti aina ya Misindano ambacho kipo katika Kituo cha Ilundi ndani ya Shamba la Miti Sao Hill. Kitalu hicho kina jumla ya miche milioni tatu kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na mingine watapewa wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo kwa ajili ya kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Displaying DSC_7386.JPG
Uchakataji wa asali katika shamba la miti Sao Hill ukiendelea. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki, Joseph Sondi na kulia ni Happyness Nandonde, Msaidizi.
*****************
Na Hamza Temba - WMU
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ina jukumu la Kuanzisha na kusimamia mashamba ya miti na manzuki za Serikali kuu, Kuna jumla ya mashamba 18 ya miti ambayo yanaendeshwa na Serikali kupitia Wakala huyo na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.

Mashamba hayo ni Buhindi, Kawetire, Kiwira, Korongwe, Longuza, Mbizi, Meru/USA, Mtibwa, North Kilimanjaro, North Ruvu, Rondo, Rubare, Rubya, Sao Hill, Shume, Ukaguru, West Kilimanjaro na Wino. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
Shamba la Miti Sao Hill ndilo shamba kubwa zaidi kati ya mashamba hayo 18 ya Serikali ambayo yanasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Kwa sehemu kubwa Shamba hilo lipo katika Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa na baadhi ya eneo katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.

Shamba hilo lilianzishwa kwa majaribio mwaka 1939 hadi 1951 na upandaji wa miti kwa kiwango kikubwa kuanza rasmi mwaka 1960 hadi 1990, Ukubwa wa shamba hilo ni Hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwa ajili ya Upandaji wa Miti (Plantation)  na Hifadhi ya Misitu Asilia (Nature Reserve).

Katika shamba hilo Jumla ya hekta 55,617.22 zimepandwa miti aina ya misindano na mikaratusi, hekta 48,200 ni maeneo ya misitu ya asili ambayo sehemu kubwa ni kwa ajili ya vyanzo vya maji, hekta 29,933 ni kwa ajili ya upanuzi wa upandaji miti na hekta 1,700 ni maeneo ya makazi na matumizi mengineyo.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala hii, Meneja wa Shamba hilo, Salehe Beleko alisema pamoja na kazi hiyo ya upandaji wa miti pia wanashughulika na ufugaji wa nyuki kama mkakati wa kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha ulinzi wa misitu na mazingira.

“Shamba letu lina jumla ya mizinga 1,298 ya nyuki na kwa mwaka 2015/16 tulivuna asali kilo 379 na baada ya kupima sampuli ya asali hiyo vipimo vya maabara vilionesha kuwa asali inayotoka kwenye hifadhi ya msitu wetu ni asali halisi isiyokuwa na kemikali (pure organic honey)” Alisema Beleko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki wa Shamba hilo, Joseph Sondi alisema katika kipindi cha Mwezi July – August, 2016 jumla ya kilo 700 za asali zimeshavunwa katika shamba hilo.

Akizungumzia dhumuni la kuanzishwa shamba hilo, Meneja Salehe Beleko alisema ilikuwa kwa ajili ya Kupunguza utegemezi wa misitu ya asili kama chanzo cha malighafi ya miti kwa matumizi mbalimbali na Kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyotumia malighafi ya miti, kwa mfano viwanda vya mbao, karatasi, viberiti, nguzo za umeme na simu.

Alisema kuwa malengo mengine yalikuwa ni pamoja na Kuboresha hali ya mazingira kwa ujumla na uoto wa asili, Kuhifadhi ardhi na vyanzo vya maji, Kuwapatia wananchi ajira zinazotokana na kazi za msimu za mashambani na kutokana na viwanda tegemezi vya mazao ya misitu pamoja na kuwa Chanzo cha mapato ya Serikali.

Akizungumzia mafanikio juu ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika shamba hilo, alisema katika mwaka wa fedha 2015/16 makusanyo yaliongezeka na kuvuka malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi bilioni 31.35 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 36.14, makusanyo ambayo ni ya juu kabisa ukilinganisha na makusanyo ya miaka ya nyuma toka kuanzishwa kwa shamba hilo.

Beleko alisema shamba la Miti Sao Hill limekuwa na faida kubwa kwa jamii ambapo kwa sasa limekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa mbao katika Wilaya ya Mufindi na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hatua hiyo inaunga mkono mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga uchumi wa viwanda.

Pamoja na faida hiyo alisema “Shamba hili limesaidia sana kuongezeka kwa ari ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wanaozunguka shamba na ukanda wote wa nyanda za juu kusini jambo ambalo limesaidia kupunguza matukio ya moto kupitia ulinzi shirikishi, Aidha limepelekea pia kupanda kwa thamani ya ardhi katika maeneo haya”.

Meneja huyo alisema Shamba hilo pia lina mchango mkubwa katika maendeleo ya Wilaya za Mufindi na Kilombero na jamii jirani ambapo wamekuwa wakipatiwa gawio la asilimia 5 ya mrahaba kila mwaka. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2000 mpaka 2016 jumla ya Mrahaba wa shilingi bilioni 4.8 umeshatolewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii hizo.

Pamoja na Mrahaba shamba hilo pia hutoa ajira mbalimbali za muda mrefu na mfupi zinazokadiriwa kufikia 34,000, ajira hizo ni katika shamba lenyewe, viwanda vya kuchakata mbao pamoja na ujasiriamali. Sehemu kubwa ya wananchi katika ajira hizo ni wakazi wa Wilaya ya Mufindi.

Akizungumzia miradi ya maendeleo, Beleko alisema Shamba hilo huchangia uendelezaji wa miradi ya maendeleo (afya, elimu, ujenzi wa ofisi za vijiji) kwa jamii zinazozunguka msitu pamoja na miradi ya upandaji wa miti na ufugaji nyuki kwenye vijiji vinavyozunguka msitu. Katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2016 jumla ya shilingi milioni 110 zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo vijiji kadhaa vilinufaika.

Miongoni mwa vijiji vilivyonufaika ni Kitasengwa, Ihalimba, Itimbo, Nyololo, Mninga, Mkalala, Vikula, Wami, Nundwe, Ibatu, Mwitikilwa, Kasanga, Changarawe, Ugesa, Ludilo na Usokami.

Katika kuboresha dhana ya ushirikishaji jamii kwenye ulinzi wa msitu, Beleko alisema “Shamba limetoa vibali kadhaa kwa vijiji na kata za Wilaya ya Mufindi katika kipindi cha miaka mitano mfululizo (2012-2016). Jumla ya miti yenye mita za ujazo 78,000 ambayo thamani yake kwa bei ya soko baada ya kuchakatwa ni shilingi bilioni 3.9, fedha hizo zimekusudiwa kwa ajili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hiyo na shughuli za maendeleo”.

Beleko alisema, kwa kuwa Shamba hilo limezungukwa na vijiji vingi, wamekuwa wakitoa mitambo ili kusaidia matengenezo ya barabara kwenye vijiji hivyo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 jumla ya kilometa 66 za barabara zimelimwa kwenye vijiji vya Kinyanambo, Itimbo-Lyasa, Ihalimba-Igomtwa-Usokami, Ugesa-Wami na Ludilo.

Aliongeza kuwa shamba hilo linatekeleza dhana ya Kilimo Mseto ambapo Wafanyakazi wa shamba na wanavijiji hugawiwa maeneo ya kulima katika maeneo yaliyovunwa miti.

“Kilimo hiki hufanyika kwa msimu mmoja tu wakati wa kupanda miti upya katika maeneo hayo. Wastani wa watu 600 hufaidika na huduma hiyo ambapo takribani tani 2,000 za mahindi yanayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 800 huvunwa kila mwaka” Alisema Beleko.

Aidha Beleko alisema, jamii zinazozunguka mashamba zinasaidiwa kwa kupatiwa mahitaji muhimu ya kuanzisha vitalu vya miche ya miti na ufugaji nyuki kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo.

“Ili kutekeleza azma hii, Shamba hugawa miche ya miti kwa jamii inayotuzunguka ambapo kwa mwaka 2014/15 jumla ya miche ya miti 300,000 yenye thamani ya shilingi milioni 120 iligawanywa na mwaka 2015/16 jumla ya miche 600,000 yenye thamani ya shilingi milioni 240 inatarajiwa kugawanywa” Alisema.

Mchango mwingine wa shamba hilo kwa Wananchi waishio jirani na shamba hilo ni fursa ya kuokota kuni kavu bure kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Vilevile wananchi wanaruhusiwa kuvuna bure mazao yasio timbao kama vile uyoga, mbogamboga na matunda. Tafiti iliyofanyika mwaka 2010 inaonesha kuwa zaidi ya kilo 80,000 za matunda aina ya pesheni (passion) yenye thamani ya shilingi milioni 240 huvunwa kila mwaka kutoka maeneo ya Shamba hilo.

Katika kutoa mchango wa huduma za afya alisema “Shamba lina zahanati moja na vituo vitatu vya huduma ya kwanza kwa ajili ya huduma ya matibabu kwa wafanyakazi na wanavijiji wanaozunguka shamba hili. Shamba huchangia katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya zahanati na vituo hivyo”.

Alisema baadhi ya vijiji vinavyonufaika na huduma hiyo ni Kihanga, Mninga, Matanana, Sao Hill, Ihalimba, Iheka, Mwitikilwa, Nundwe, Vikula, Kitasengwa na Makungu. Kwa wastani jumla ya wananchi 2,000 kutoka kwenye vijiji vinavyozunguka Shamba hupata huduma ya matibabu kutoka kwenye zahanati ya Shamba na vituo vyake.

Katika mchango wa elimu, Shamba lina shule ya msingi moja ambayo hutoa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wa shamba, kiwanda cha mbao cha Sao Hill na jamii inayozunguka shamba. Shamba kwa kushirikiana na uongozi wa kiwanda cha mbao cha Sao Hill linahudumia shule kwa kuwapatia walimu nyumba za kuishi, madarasa ya wanafunzi na ukarabati wa majengo yote pamoja na huduma nyingine muhimu kama vile maji, umeme, usafiri na matibabu.

Aidha Beleko alisema kuwa katika kuunga mkono sera ya Serikali ya awamu ya tano ya elimu bure, jumla ya madawati 4,112 yanatengenezwa kwa ajili ya kutatua changamoto ya uhaba wa madawati katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla. Alisema madawati hayo yakikamilika yatakabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi.

Akizungumzia kuhusu kukua kwa uchumi wa Mji wa Mafinga Beleko alisema Biashara ya Magogo na Mbao imepelekea Mji wa Mafinga kukua kwa kasi kiuchumi hadi kupewa hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo. Takribani asilimia 62 ya watu wenye vibali vya kuvuna miti na kuchakata magogo katika shamba la miti la Sao Hill ni wenyeji wa wilaya ya Mufindi kutoka katika vijiji vinavyozunguka msitu.

Beleko alisema kuwa pamoja na faida zote hizo shamba linahitaji gharama kubwa za uendeshaji ili liweze kuzalisha ipasavyo ambapo bajeti yake kwa mwaka ni takribani shilingi bilioni 10 mpaka 15.

Kuhusu fursa za uwekezaji katika shamba hilo, Beleko alisema uwepo wa shamba umeipa fani ya Misitu umaarufu mkubwa Wilayani Mufundi na Ukanda wote wa Nyanda za Juuu Kusini, Hivyo kutoa fursa ya uwekezaji katika viwanda na vyuo mbalimbali vya Misitu kwa ajili ya kuzalisha wataalamu katika fani hiyo.

Alisema fursa nyingine ni pamoja na ufugaji wa nyuki kutokana na uwepo wa misitu ya asili, ya kupandwa pamoja na vyanzo mbalimbali vya maji. Alieleza kuwa asali inayozalishwa katika shamba hilo ilipimwa katika moja ya maabara ya kimataifa nchini Ujerumani na kuthibitika kuwa haina kemikakali yeyoye (pure organic).

“Fursa ya kuwekeza katika viwanda vya maji pia inapatikana katika shamba hili kutokana na uwepo wa chem chem na vyanzo mbalimbali vya maji. Yapo pia maporomoko ambayo yanafaa kwenye nishati ya umeme wa maji pamoja na mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki, tunawakaribisha wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta hizo” Alisema Beleko.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki, Joseph Sondi alisema pamoja na shughuli za uzalishaji wa mazao ya misitu na asali, Sao Hill pia ni Kituo cha Mafunzo kwa vitendo ambapo kila mwaka hupokea wanafunzi mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Sokoine (SUA), Dar es Salaam (UDSM) na Mipango Dodoma. Vilevile mashamba mapya ya miti yaliyoanzishwa kama vile Wino na Mbizi hujifunza katika shamba hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Festo Elia Mgina alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia mahusiano baina ya shamba la Sao Hill na Halamshauri yake alisema, uwepo wa shamba hilo umeongeza mzunguko mkubwa wa fedha na ajira katika Halmashauri hiyo.

“Siasa za Mufindi ni Sao Hill, mtu mmoja anayenunua mita za ujazo 200 ambazo ni kiwango cha chini kabisa anaajiri watu wasiopungua 40 katika mfumo mzima wa uchakataji jambo ambalo linaongeza ajira kwa wakazi wa mufindi na wakati huo huo mzunguko mkubwa wa fedha” Alisema Mgina.

Aliongeza kuwa shamba hilo limehamasisha kwa kiwango kikubwa upandaji wa miti kwa jamii inayolizunguka ambapo pia hutoa msaada wa mafunzo na miche ya miti kwa ajili ya kupandwa. “Hamasa ya kupanda miti imekuwa kubwa kutokana na thamani inayoonekana Sao Hill kiasi kwamba imefikia hatua sasa tunawaelimisha watu wetu waache baadhi ya maeneo kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara” Alisema Mgina.

Akizungumzia misaada mingine inayotoka Sao Hill alisema ni pamoja na elimu ya kukabiliana na moto ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuondoa tatizo hilo, Msaada wa mitambo ya kutengeneza barabara na vifaa mbali mbali vya ujenzi, zahanati na mashule.
Posted by MROKI On Friday, September 23, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo