Neema Arora akiwa ofisini kwake.
KATIKA kipindi cha miaka mingi iliyopita jamii nyingi za Kiafrika
ikiwemo Tanzania mfumo dume ulitawala kwa kiasi kikubwa. Hali hii
imechangia wanawake kubaki nyuma katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Chini ya mfumo huu, wanawake wengi wamekosa fursa ya kupata elimu na
wachache waliobahatika kupata elimu walikuwa hawaaminiwi kupatiwa nafasi
za kutoa maamuzi ikiwemo uongozi kwa ujumla.
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo na mabadiliko ambayo
taratibu yameanza kuundoa mfumo dume ambapo hivi sasa wanawake
wameanza kuchomoza na kufanikiwa kupata elimu inayowawezesha kupata nafasi za
kufanya kazi za kitaaluma ambazo kwa miaka mingi zilikuwa zikishikiliwa na
wanaume pekee ikiwemo kupata fursa za uongozi japo idadi bado ni ndogo kwa
kulinganisha na wanaume.
Ili kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma serikali za nchi mbalimbali za
Kiafrika ikiwemo Tanzania zimeanza kuhamasisha na kutekeleza mpango wa Elimu
kwa Wote ambao kwa kiasi kikubwa umeonyesha kuleta mafanikio pia taasisi zisizo
za kiserikali zimeanzisha programu mbalimbali za kuwapatia mafunzo mbalimbali
ya kuwajenga uwezo wa kujiamini zaidi.
Moja ya Programu ambayo imeanzishwa hapa nchini katika miaka ya
karibuni kwa ajili ya kuwanoa wanawake wasomi kujifunza masuala ya Utawala na
uongozi kwenye bodi za makampuni inajulikana kama ‘Mwanamke Wa Wakati
Ujao’ au kitaalamu kama Female Future Programme. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Tangu Programu hii ianzishwe, taasisi na makampuni
mbalimbali makini ambayo yanazingatia usawa wa kijinsia tayari
yameanza kufadhili wafanyakazi wake wanawake kupata mafunzo yanayotolewa chini
ya mpango huu.
Moja ya kampuni ambayo imekuwa mstari wa
mbele kutekeleza mpango wa kuwawezesha wafanyakazi wake wanawake ambayo
imeanza kuwapatia fursa wafanyakazi wake kuhudhuria mafunzo ya Programu ya ‘Mwanamke
Wa Wakati Ujao’ ni TBL Group.Kampuni hii pia imekuwa ikitekeleza mpango wa
uwezeshaji wanawake ndani ya kampuni ujulikanao kama TBL Women’s Forum (TWF).
Mmoja wa wafanyakazi wa TBL Group,Neema Arora (pichani chini na Juu) mwenye nafasi ya
Meneja wa upishi wa Bia (Brewing Manager) katika kiwanda cha DarBrew ni
miongoni mwa wanafunzi wa kozi ya Female Future Programme.
Katika mahojiano hivi karibuni alianza kwa kushukuru mwajiri wake
kwa kumpatia fursa ya kupata mafunzo yanayotolewa kupitia mpango huu na
alieleza kuwa kwa muda mfupi tangia ajiunge nayo ameweza kujifunza mambo
mengi ya utawala ambao hakuyajua kabla pia yamemuongezea kujiamini katika
utendaji wake wa kazi wa kila siku.
Katika Programu hii alisema wanafundishwa masuala mengi hususani
utawala wenye kuleta ufanisi kwa makampuni,kujiaamini na jinsi ya kushiriki na
kuchangia mawazo katika vikao vya juu vya bodi za makampuni “Mtaala wa
kufundishia unaotumika ni mzuri na ndani ya kipindi cha muda mfupi
unaweza kumbadilisha mtu kuwa na maarifa na upeo mkubwa na kujiamini.
Jukwaa hili ni fursa pekee kwa Wanawake ambao bado hawapati fursa kubwa za
uongozi hususani katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania”,alisema.
Bi.Lilian Machera kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambaye
anairatibu kozi hii alisema inaendeshwa ATE kwa ushirikiano na taasisi ya
Confederation of Norwegian Enterprises ya nchini Norway (NHO) ambayo
dhumuni lake ni kuwapatia wanawake walioajiriwa katika makampuni mbalimbali
mafunzo ya uongozi wa juu katika makampuni hayo na kuwajengea uwezo wa kuweza
kushiriki katika vikao vya juu vya bodi. Alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo umebainisha kuwa ni
wanawake asilimia 35% ndio wanashikilia nafasi za uongozi wakati wanaume
wanashikilia asilimia 65%.
Alisema mafunzo haya kwa hapa nchini yanaendeshwa kwa kushirikiana na
chuo cha Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI)
kilichopo mkoani Arusha na zaidi ni ya vitendo kuliko nadharia “Wanafunzi
wanaojiunga na mafunzo ya mpango huu wanaweza kukutana darasani katika siku 14
ndani ya kipindi cha miezi tisa zaidi ya hapo wanakuwa wanajisomea na
kufanya kazi kwa vitendo katika sehemu zao za kazi na wanapofikia mwisho wa
mafunzo wanafanya mitihani na kutunukiwa vyeti kwa wale wanaofaulu”.Alisema
Machera.
Kwa upande wake Mratibu mwenza wa Programu hii kutoka taasisi ya
Confederation of Norwegian Enterprises (NHO),Mavie Bordvik amesema
anafurahi kuona progamu hii imeanzishwa hapa nchini. “Mpango wa mafunzo haya
tayari umenufaisha wanawake zaidi ya 200 katika nchi ulipoanzia zikiwemo nchi
za Nigeria,Kenya na Uganda.
Alisema nchi nyingi hususani zinazoendelea mfumo dume umetawala
kwa muda mrefu kiasi kwamba kunahitajika jitihada za kuuondoa na
kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa na wanaume au zaidi kwa kuwa
wanao uwezo wa kufanya lolote na jinsia yao haiwaondolei uwezo wa kufanya mambo
makubwa yanayofanyika hapa duniani ikiwemo kushika nafasi za juu za uongozi na
kutoa mawazo na maamuzi magumu.
Bi.Zuhura Muro,mwanamke msomi aliyebobea katika maswala ya
Raslimali Watu na Utawala ambaye amekuwa akishikilia nyadhifa za uongozi
kwenye bodi za makampuni mbalimbali akiongelea juu ya mpango huu katika
mahojiano maalum alisema “ Mpango wa kuwapatia wanawake mafunzo ya
utawala ya Female Future Programme ni moja ya jukwaa la kuwanyanyua wanawake wa
Tanzania na kuwafikisha kwenye nafasi za juu za uongozi na kutoa maamuzi”.
Alisema bado kuna idadi kubwa ya wanawake
wasomi nchini wanaohitaji kujengewa uwezo wa kushika nafasi za juu za uongozi
na kushiriki kutoa maamuzi kwenye vikao vya bodi za wakurugenzi wa makampuni na
kuna haja ya kuanzishwa mafunzo ya aina haya mengi ili wanawake wengi waweze
kufikiwa kwa haraka na kutoa mchango wao katika kuleta maendeleo kwa
taifa.
“Tafiti mbalimbali za kitaalamu zinabainisha wazi kuwa kampuni au
taasisi yoyote inayoshirikisha wanawake katika ngazi za uongozi kwa
vyovyote itafanya vizuri na kupata mafanikio kwenye shughuli zake kwa kuwa
wanawake ni wepesi wa kujifunza na kutumia ujuzi wao wanaoupata kwa umakini na
wanayo dhamira ya kudhihirisha kuwa wanao uwezo wa kufanya mambo makubwa na
alishauri wapewe nafasi za juu waonyeshe uwezo wao badala ya kuachwa
nyuma.
“Licha ya changamoto zinazowakabili wanawake katika mzunguko wao wa
maisha ambao wenzao wa jinsia ya kiume hawazipati ni muhimu wapewe fursa
kwa kuwa wana uwezo”.
Alimalizia kutoa wito kwa wanawake wote wa Tanzania kuamka na
kuchangamkia fursa za kujiendeleza zinapojitokeza na kuachana na mawazo ya
kujiona wanyonge mbele ya wanaume.
0 comments:
Post a Comment