Waziri wa Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Gerson Lwenge akifungua kikao cha pamoja na ujumbe wa Benki ya
dunia, Wizara ya Maji ,Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam
(Dawasco ) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasa)
namna ya kutatua changamoto za usambaza Maji kwenye Jiji la Dar es Salaam
yakiwamo Mivujo na Miundombinu chavu , kilichofanyika Jijini Dar es salaam.
************
Dar es Salaam.
KATIKA kuhakikisha sekta ya
Maji inakua kwa kasi na inatosheleza mahitaji ya sasa ya huduma ya maji, Benki
ya Dunia imejitolea kulisaidia Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es
salaam (DAWASCO), ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma ya Majisafi na
Majitaka katika maeneo mbalimbali ya wakazi wa jiji la Dar es salaam pamoja na
Miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.
Hayo yamezungumzwa na
Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bi. Bella Bird, ambaye alikuwa ameambatana
na wajumbe wake katika kikao cha pamoja na Waziri wa Maji, Mhandisi Gerson
Lwenge, pamoja na Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam
(DAWASCO).
Kikao ambacho kililenga
uboreshaji na upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo kadhaa ya jijini Dar
es Salaam hasa maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.
Aidha, Mwakilishi huyo wa
Benki ya Dunia, ameridhishwa na juhudi za makusudi zinazofanywa na Dawasco
katika kuwapatia wananchi huduma ya Majisafi, pamoja na kupambana na kiwango
cha Maji kinachopotea bila sababu ya msingi.
Ameeleza kuwa Benki ya dunia
imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Majisafi na Majitaka ili
kuimarisha uendeshaji wa utoaji wa huduma ya Maji kwa wananchi, ikiwa ni pamoja
na kutekeleza kikamilifu kampeni ya “Mama Tua Ndoo Kichwani” ili kuwapunguzia
akina mama wengi tatizo la Maji, kwani ndio wanaoonekana kuwa wahanga wakuu wa
tatizo hilo.
“Nimeridhishwa na utendaji
wenu wa kazi, jinsi ambavyo mmejipanga katika kufanya kazi, hasa juhudi zenu
mnazoziweka katika kupambana na upotevu wa Maji na kuwapatia wananchi huduma ya
Maji” alisema Bi. Bird
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa
Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano
mzuri waliouonesha, na kwamba kiasi cha fedha kilichotengwa na Benki ya Dunia
kitatumika katika kuboresha na kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili
shirika katika utoaji wa huduma ya Maji.
“Changamoto ni nyingi katika
utoaji wa huduma ya Maji, naamini kuwa kiasi cha fedha kilichotengwa kitasaidia
kuondoa changamoto hizo” alisema Mhandisi Luhemeja.
Benki ya dunia imekuwa
ikifadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwamo miradi mbalimbali
katika sekta ya Maji, Nishati na Madini, Kilimo na Mifugo, pamoja na Uchumi na
Biashara.
0 comments:
Post a Comment