ISO 9001:2008
CERTIFIED
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI KUHUSU KODI
YA ONGEZEKO LA THAMANI KWENYE
HUDUMA ZA KIFEDHA (VAT ON FINANCIAL SERVICES)
Bunge
la Tanzania limepitisha marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) ya mwaka 2014 kuanzia tarehe 1 Julai 2016 kwenye huduma za kifedha kwa
kurekebisha kifungu cha 13 cha Jedwali la Msamaha wa kodi.
Lengo la tamko hili ni
kufafanua utozwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za kifedha kwa-
a)
Kujulisha umma, Benki, Taasisi za Fedha na wadau
wote kuhusu maudhui na utekelezaji wa sheria hii inayolenga kutoza Kodi ya Ongezeko
la Thamani kwenye huduma za kifedha;
b)
Kuondoa utata na upotoshaji unaohusu utekelezaji
wa sheria hii inayoanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2016; na
c)
Kuelezea ukweli kuhusu utekelezaji wa sheria
iliyopitishwa na Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao
chake cha 3.
Sheria hii inalenga kutoza Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia 18 kwenye ada (fees) ambazo benki inatoza wateja wake
kwenye huduma mbalimbali zitolewazo na benki au taasisi za fedha.
Kuna taarifa ambazo si za
kweli zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa VAT itatozwa kwenye amana
ya mwenye fedha kwenye benki. Hii siyo
kweli. Ukweli ni kuwa kiasi cha VAT kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha
gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha.
Mfano: Ada
(fees) ya huduma ya benki ambayo
mteja ametozwa ni Shilingi 1000/=, Kodi ya Ongezeko la Thamani itakayotozwa
kwenye kiasi hiki ni shilingi 152.50 tu na benki kubaki na shilingi 847.50. Kiwango
hiki cha shilingi 152.50 ndicho kitakachorejeshwa serikalini na benki au taasisi
ya fedha baada ya kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani iliyolipwa kwenye
manunuzi ambayo yamefanywa na benki au taasisi ya fedha husika. Kwa mujibu wa
sheria hii, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) haitatozwa kwenye riba inayotozwa
na benki kwenye mikopo.
Aidha kuna maelekezo
yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji wa huduma za kifedha
atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala husika haukupitia kwenye
akaunti. Taarifa hii si sahihi kwa kuwa ukusanyaji wa VAT husika utafanywa kwa
njia ile ile ambayo gharama za huduma za kifedha zinakusanywa sasa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania itatoa
maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielekroniki utakavyofanyika ili
kuiwezesha benki au taasisi ya kifedha kutimiza matakwa ya kisheria ya Kodi ya Ongezeko
la Thamani ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Hivyo, kupitia taarifa hii,
tunazitaka Benki na Taasisi za Fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa taarifa
zisizosahihi kwa umma kuacha mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria
zitachukuliwa. Kimsingi, benki na taasisi za fedha zinazohusika zinaagizwa
kurekebisha mara moja taarifa walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi
ya marekebisho ya Sheria hii.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
A. J. Kidata
KAMISHNA MKUU
MAMLAKA YA MAPATO
TANZANIA.
0 comments:
Post a Comment