BAADA ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0
katika mechi zake mbili za kimataifa , timu ya soka ya Vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebakiza mitihani miwili kabla ya kuandika
historia ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, imefahamika.
Mtihani wa kwanza ni mchezo dhidi ya Afrika Kusini
unaotarajiwa kufanyika ama Agosti 5, 6 au 7, 2016 ambako mechi ya kwanza
itapigwa ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam, Tanzania wiki moja
baada ya mchezo huo. Hivyo mchezo wa marudiano utafanyika Uwanja wa Azam
Complex, ulioko Chamazi Agosti 14, 2016 saa 9.00 alasiri.
Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu
mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville. Wakati Afrika Kusini imepitishwa
moja kwa moja Namibia imepenya kwa kuiondoa Botswana licha ya kufungwa mabao
2-1 katika mchezo wake uliofanyika jana Julai 2, 2016 huko Botswana.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Namibia, Juni 24,
mwaka huu wenyeji (Namibia) walishinda 1-0. Kwa msingi huo, Namibia imepenya
kwa bao la ugenini ililolivuna katika mchezo wa jana. Bao la ugenini imefanya
kuwa na mabao 3-2.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Nyundo Shime, ameangalia
ratiba ya mlolongo huo na kusema “Ushindani utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga
kushinda michezo yote iliyo mbele yangu. Si kwamba napigania kufuzu kwenda
Madagascar tu kwenye fainali za Afrika, la hasha, nataka timu hii niipeleke
Kombe la Dunia.”
Fainali za Kombe la Dunia, mwakani zitapigwa India
ambako kama Serengeti Boys itafuzu kucheza fainali za Afrika na ikaingia nusu
fainali kwa maana timu nne bora zote zitashiriki fainali hizo ambazo tayari
Tanzania imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.
“Timu hii nimeanza nayo zaidi ya mwaka mmoja. Sioni kama
itakuwa kikwazo kuifanikisha kufika fainali za Kombe la Dunia. Namuomba Mungu
atunyooshee mkono wake, nawaombea viongozi wa TFF wazidi kuihudumia timu hii,
lakini pia wadau wengine waisapoti timu hii bila kuangalia au kuchagua mtu
anayeongoza TFF. Hii ni timu ya Watanzania wote,” amesema Shime maarufu kama
Mchawi Mweusi.
Shime alishukuru mipango na ahadi ya Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kugharamia kambi ya wiki mbili
itakayofanyika Madagascar kuanzia Julai 24, mwaka huu akisema: “Hii itakuwa ni
kambi bora. Kwa sasa kikosi change kinahitaji utulivu hivyo kwa maoni na
mipango yangu naona inafaa.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu kwa
Vijana anayeongoza timu hiyo, Ayoub Nyenzi kadhalika aliomba sapoti ya
Watanzania ili kuendeleza timu hiyo, amesema: “Hakika nikipata watu
wakatusapoti, naamini ndoto zangu zitatimia .”
Nyenzi amethibitisha kwamba timu hiyo itaondoka hapa
jijini Victoria kesho Jumatatu Julai 4, 2016 saa 11.00 jioni Kisiwa cha Mahe miongoni mwa visiwa 115 vya
nchi hii ya Shelisheli na inatarajiwa kufika Tanzania saa 7.45 usiku wa kuamkia
Jumanne Julai 5, mwaka huu.
“Wachezaji watakuwa na mapumziko mafupi kabla ya kuanza
kambi ya maandalizi kwenda Madagascar kwenye kambi ya kuiandaa timu kucheza na
Afrika Kusini,” amesema Nyenzi ambaye pia alijibu kuwa watawapumisha nyota hao
kwa ushauri wa makocha na daktari: “Mapumziko mafupi. Msihofu”
Timu hiyo yenye wachezaji 20 na viongozi wanane, itasafiri
kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia hadi kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kubadili ndege ya kuunganisha
kwenda Dar es Salaam, Tanzania. Ikiwa Shelisheli ilifikia hoteli ya Berjaya
Beau Vallon Resort, iliyoko jijini Victoria. Hoteli ipo umbali wa Kilometa 25
kutoka uwanja wa ndege.
Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm
Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari,
Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally
Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi,
Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin
Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid
Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima
Makame Vitalis.
Hivi karibuni Serengeti Boys ilifanya ziara India
ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA
(AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya
kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika
nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
0 comments:
Post a Comment