Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni jijini Kampala mara baada ya kumalizika kwa sherehe za uapisho wa Rais Museveni.
**************
RAIS wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 12 Mei, 2016 amefanya mazungumzo
na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni muda mfupi baada ya
kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais huyo iliyofanyika katika uwanja wa
Kololo Jijini Kampala.
Katika Mazungumzo hayo Rais
Magufuli amempongeza Rais Museveni kwa kuapishwa kuwa Rais wa Uganda kwa
kipindi kingine cha miaka 5 na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na
kukuza zaidi Uhusiano, ushirikiano na udugu wa kihistoria uliopo kati ya nchi
hizo.
Viongozi hao pia wamezungumzia
mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima (Ziwa Albert) nchini
Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania ambapo pamoja na kuishukuru Uganda
kwa uamuzi wake wa kuamua bomba hilo lipitie Tanzania, Rais Magufuli amemshauri
Rais Museveni kufupisha muda wa ujenzi wa mradi huo, kwa kutumia mbinu
inayojumuisha usanifu na ujenzi (Design
and Construct method) na kutumia wakandarasi wengi watakaogawanywa katika
vipande tofauti badala ya kutumia mkandalasi mmoja.
"Nashauri tutumie mbinu ya
usanifu na ujenzi pamoja, hii ni njia ya haraka zaidi, na pia tugawe vipande
vya ujenzi kwa njia yote ya bomba la mafuta yenye urefu wa kilometa 1,410
tunaweza kuwa na Wakandarasi watano mpaka sita ambao watatumia njia hiyo mpya
ya usanifu na ujenzi. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
"Kwa kufanya hivyo tutakuwa
tumepunguza muda utakaotumika kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta, inaweza
hata kuchukua mwaka mmoja tu" Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amebainisha kuwa
kwa kufanya hivyo faida za mradi huo wa mafuta zitaanza kupatikana mapema
badala ya kusubiri miaka miwili au mitatu ijayo, na kwamba hiyo itakuwa
inaendana na kauli mbiu yake ya "Hapa Kazi Tu"
Pia Rais Magufuli amemshukuru
Rais Museveni kwa uamuzi wa nchi hiyo wa kuipa Tanzania umiliki wa asilimia 8
katika mradi huo wa bomba la mafuta.
Kwa upande wake Rais Museveni
amesema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, na
pia amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa ambazo amezifanya katika
mapambano dhidi ya rushwa nchini Tanzania.
"Napenda kasi yako ya
uongozi, napenda jinsi unavyopambana na rushwa, kwa sababu rushwa ilikuwa
inazaa matatizo mengine kama vile ucheleweshaji wa mizigo bandarini na vikwazo
vya mpakani, hivyo nakupongeza sana kwa hilo" Amesema Rais
Museveni.
Katika sherehe ya kuapishwa
kwa Rais Museveni iliyofanyika kabla ya mazungumzo hayo, pamoja na Rais
Magufuli viongozi wengine kutoka Tanzania waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa
awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete aliyekuwa na Mkewe Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Suzan
Kolimba.
0 comments:
Post a Comment