Mbunge wa jimbo la Iramba Bw Mwigulu Nchemba wa pili kushoto akikabidhi bati zaidi ya 450 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu ,zahanati na nyumba vya madarasa
Wananchi wa jimbo la Iramba wakimpongeza mbunge wao Bw Nchemba kwa utekelezaji wa ahadi zake
Na MatukiodaimaBlog
MBUNGE wa jimbo la Iramba wilayani Iramba mkoani Singida Bw Mwigulu Nchemba ameendelea kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi wake kwa kumchagua kwa kishindo katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 kwa kutekeleza ahadi mbali mbali alizopata kuwaahidi wakati wa kampeni .
Mbunge Nchemba amekabidhi bati hizo jana wakati wa mikutano yake ya kuwashukuru wananchi wake wa jimbo la Iramba kwa kumchagua na kuanza utekelezaji wa ahadi zake.
Alisema kuwa lengo la kuanza kukabidhi ahadi zake ni kuwafanya wananchi kuharakisha ukamilishaji wa shughuli za kimaendeleo jimboni hasa katika nyanja ya elimu na afya na kuwa bati hizo zitasaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa ,nyumba za walimu na Zahanati .
Kwani alisema ndoto yake ya mbeleni ni kuona jimbo la Iramba na wilaya ya Iramba inaendelea kuwa mbele katika ubora wa vyumba vya madarasa na wengine kufika kujifunza Iramba
Hivyo alisema pamoja na kuchangia bati kwa ajili ya ujenzi huo bado atajitolea kununua tofari za kujengea ambazo kwa kila kijiji vijana watafyatua na yeye atazinunua kwa bei ambayo wao watataka kama sehemu ya kutoa ajira kwa vijana vijijini pia vifaa vyote vya viwandani kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ni juu yake wananchi wanachotakiwa kufanya ni kushiriki katika shughuli za kimaendeleo .
Pia aliwataka walimu na watumishi wanaopangwa kufanya kazi katika wilaya ya Iramba kujenga utamaduni wa kupenda kufanya kazi katika wilaya hiyo badala ya kuripoti na kuondoka .
Nchemba ambae ni waziri wa kilimo ,mifugo na uvuvi alisema kuwa vipaumbele vyake kwa wananchi wake ni maji na umeme ambavyo tayari umeme umeanza kusambazwa vijijini pia maji anaendelea jitihada japo alisema suala la Miundombinu bado ni changamoto .
Wakati huo huo waziri Nchemba ameshauri uongozi wa Halmashauri kuruhusu wanafunzi wanaopata matatizo ya ugonjwa wakiwa shuleni kupatiwa matibabu ya bure katika vituo vya afya ,Hospitali na zahanati katika jimbo hilo badala ya kuwarudisha nyumbani .
Alisema kuna haja ya Halmashauri kupitia vyanvzo vyake vya ndani kusaidia kuwalipia matibabu wanafunzi hao na kuwa ofisi yake itasaidia kufidia pesa hizo kwa kugharamia baadhi ya miradi ambayo inapaswa kutekelezwa na Halmashauri kama ambavyo anafanya sasa kwa kujitolea kujenga vyumba vya madarasa na Zahanati .
0 comments:
Post a Comment