Nafasi Ya Matangazo

March 17, 2016

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) inatarajia kutoa hukumu ya rufaa ya kesi ya mauaji na wizi wa kutumia silaha inayowahusu raia 10 wa Kenya itakayotolewa  kesho Ijumaa ( Machi 18, 2016) katika makao makuu ya mahakama hiyo yaliyoko jijini Arusha, Tanzania. Anaandika Na Kulwa Mayombi, EANA.
Raia hao wa Kenya walikutwa na hatia ya kosa la mauaji na ujambazi wa kutumia silaha lililofanyika katika benki  ya  NMB Tawi la Moshi mwezi May,2004.
Washtakiwa hao, Wilfred Onyango na wenzake 9, wamepinga mashtaka hayo.
Watu hao walilalamika kuwa Januari 2006, walisafirishwa kwa ndege ya kijeshi na kurejeshwa Tanzania kutoka Msumbiji na kufunguliwa mashtaka ya mauaji na mashtaka 3 ya wizi wa kutumia silaha. Wanadai kuwa walikuwa Msumbiji kihalali kwajili ya shughuli za kibiashara.
Wanaitaka mahakama ya Afrika, pamoja na mambo mengine, kuelekeza mamlaka husika iliyowatia hatiani kufuata mchakato wa kisheria katika kesi yao na kutaka malipo yatolewe kwa kudhalilishwa utu wao.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imepinga madai ya walalamikaji hao na kuitaka mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya walalamikaji hao.
Katika kikao chake cha kawaida cha 37 kilichofanyika jijini Arusha May, 2015  majaji wa mahakama hiyo ya haki za binadamu na watu walisikiliza maombi  ya walalamikaji hao.
Mahakama hiyo ina jumla ya majaji 11 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika waliochaguliwa na nchi zao kutumikia mahakama hiyo .
Vikao vya kawaida vya mahakama hiyo hufanyika mara 4 kwa mwaka, lakini pia huweza kufanyika katika wakati usio wa kawaida kutegemea na suala la kutazamwa.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi februari 2016, Mahakama imepokea kesi 74 na kesi 25 kati ya hizo zimekwisha shughulikiwa huku kesi 4 zikipelekwa katika Tume ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu nchini Gambia.
Posted by MROKI On Thursday, March 17, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo