RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amelaumu Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) kwa kutumia pesa ‘kiholela’ kutokana na mawaziri kufanya
ziara za mara kwa mara kuhudhuria mikutano.
Amesema mawaziri wa nchi yake wanatumia chombo
hicho kama njia ya kujinufaisha kwa kufanya ziara na kuhudhuria mikutano ya
jumuiya hiyo isiyo muhimu.
Rais Kagame ameahidi kuiga mfano wa Rais John Magufuli
wa Tanzania kutokomeza ufisadi huo kwa
kusitisha ziara za mawaziri alizotaja kuwa za kufuja mali ya taifa.
Akiongea katika mkutano wa faragha wa viongozi wa
taasisi zote za serikali nchini Rwanda, Rais Kagame amesema suala la ufisadi
nchini humo linachukua mwelekeo mpya na kasi ya ajabu na kwamba hawezi
kuendelea kuvumilia.
Rais Kagame alisema EAC imeanza kuwa ghali na mzigo kwa taifa
lake akisema mawaziri katika mataifa wanachama wanatumia jumuiya hiyo kama
chombo cha kuchota pesa kwa kubuni mikutano ya kila siku baadhi akiitaja kuwa
haina umuhimu wowote.
Alisema mawaziri wake wasiopungua watano
wanasafiri kama mara tatu kwa wiki kushiriki mikutano ya EAC popote inapotokea
katika nchi wanachama na kwamba ziara hizo zinaigharimu serikali fedha nyingi.
“Ni kama mawaziri wa nchi hizi walikubaliana
kushinikiza serikali zao kuwa lazima wahudhurie kila aina ya vikao vya jumuia
hii kwa kisingizio kuwa waziri anayeshindwa kuhudhuria nchi yake inachukuliwa
hatua ama inaonekana kupinga juhudi na mikakati ya jumuiya,” alisema Rais
Kagame.
Moja ya njia alizosema anaweza kutumia ni kumpa
waziri wake wa masuala ya EAC, Valentine Rugwabiza jukumu la kushughulikia
masuala yote yanayohusu jumuiya hiyo.
Amepongeza juhudi za Rais wa Tanzania John
Magufuli za kukomesha ufisadi uliokuwa umekithiri katika taasisi za serikali,
akisema lazima na yeye afuate nyayo za Rais Magufuli katika suala zima la
kukomesha ufisadi na ufujaji wa mali ya serikali.
Rwanda inaorodheshwa ya kwanza katika nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana anasema miaka ya
nyuma viongozi kadhaa wa wilaya na taasisi nyingine za serikali walipoteza kazi
zao na kutupwa jela kwa makosa ya kuhusika na rushwa na ufisadi.
0 comments:
Post a Comment