“Tatizo la ajira nchini limekuwa
likiongezeka hapa nchini mwaka hadi mwaka ila wanawake wengi ndio hawana kazi
wameachwa nyuma katika sekta zote kiasi kwamba kunahitajika ushawishi wa ziada
wa kuwahimiza watoto wa kike nchini kuachana na kasumba ya kuchagua
kazi”Anasema Imelda Myovela ,mfanyakazi wa kiwanda cha TBL Arusha ambaye ni
mwanamke pekee fundi wa umeme.
Myovela anaendelea kueleza kuwa iwapo watoto wa kike hawatapata
ushawishi wa kuwaeleza kuwa masomo yote wanayaweza wanapokuwa mashuleni na wana
uwezo wa kufanya kazi yoyote inayofanywa na wanaume kuna hatari ya wanawake wa
Tanzania kuendelea kubaki nyuma kwa kuachwa nje ya mfumo wa ajira.
Alisema jambo la kusikitisha hata watoto wa kike wengi wanaosoma masomo
ya ufundi mara nyingi wanabadilisha kazi na wengine kuamua kukaa bila kazi kwa
kuogopa kufanya kazi walizosomea na hali hiyo ndio inasababisha kila sehemu ya
kazi hususani za kawaida kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaume.
Akielezea historia ya elimu yake Imelda anasema baada ya kuhitimu
masomo yake ya sekondari mwanzoni mwa miaka ya
themanini alijiunga na Chuo cha VETA cha Dar es Salaam ambapo alisoma
kozi ya ufundi wa umeme wa viwandani. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Baada ya kuhitimu kozi hiyo na kufanya mafunzo ya vitendo,mwaka 1983
alifanikiwa kupata ajira katika kampuni ya TBL ya Dar es Salaam ambako
ameajiriwa kama fundi umeme hadi kufikia sasa.
“Kufanya kazi katika kampuni hii kumeniwezesha kuwa na ujuzi mkubwa
katika fani hii ikizingatiwa kuwa kuna mafunzo mengi tunapata ambayo huwezi
kuyapata chuoni pia kampuni imefunga mitambo ya kisasa na inayotumia teknolojia
ya juu hivyo inahitaji uwe umebobea katika fani kwendana na mazingira ya
kazi”.Alisema.
Aliongeza kwamba anajivunia kazi yake japo wenzake wote anaofanya nao
kazi ni wanaume na anafurahi kuona anaimudu na anaaminiwa na mwajiri wake kama
wanavyoaminiwa wafanyakazi wanaume.
Kuhusu changamoto anazokabiliana
nazo katika kazi yake alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo kwenye
kazi nyingine . “Hakuna kazi isiyokuwa na changamoto kwa kazi kama hii ya
kwangu unapokuwa na watoto wadogo na kufanya kazi za shift unakuwa na wasiwasi
hata hivyo namshukuru mme wangu ni muelewa amekuwa akinisaidia na kunitia
moyo”.Alisema
Imelda ambaye ni mama mwenye watoto watatu anasema kuwa anafurahi kufanya
kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye
maslahi mazuri ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara
wafanyakazi wake na anakiri kuwa ajira
yake imemwezesha kupata mafanikio kimaisha mojawapo ikiwa ni kuwasomesha watoto
wake kwenye shule nzuri .
“Kwenye kampuni kama hizi tunafundishwa mambo mengi ambayo hata
yanakunufaisha ukiwa nyumbani kwako kama vile usafi wa mazingira pia kupanga
bajeti kwa kila kitu unachofanya”.Alisema
Kuhusu mipago yake ya baadaye alisema kwa sasa hana mpango wa
kubadilisha kazi na itakapofikia wakati wa kustaafu ataendelea kufanya shuhuli
zake binafsi za kujiajiri.
Alimalizia kwa kuwataka akina
mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote bila kuchagua kwa kuwa hakuna
kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake peke yao na hakua kazi rahisi
kila kazi ina changamoto zake. “Akina mama tuamke na watoto wa kike
changamkieni masomo ya ufundi ili muweze
kupata ajira nzuri zitakazowawezesha kuboresha maisha yenu”.Alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment