Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2016

WIZARA YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWATUMIA WAHITIMU WA VYUO VYA KILIMO WALIOSOMA KOZI MAALUM

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi inautangazaia umma kuwa wahitimu mahiri 10,629 waliofuzu Vyuo vya Kilimo vya Inyala, Mtwara, Horti Tengeru, Igurusi, Katrin, Ukiriguru, Maruku, Uyole, KTC Moshi, Mlingano, Tumbi, Ilonga, NSI Kidatu  na Mubondo, wanaweza wakatumiwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.

Jumla ya wahitimu 7,525 wamefaulu katika ngazi ya Astashaada kati ya hao, wanawake ni 2,557 na wanaume ni 4,968. Wahitimu 3,104 wameafaulu katika ngazi  ya Stashahada (Diploma) ambapo  wanawake ni 774 na wanaume 2,370.

Wahitimu hawa ni mahiri katika michepuo ya Stashahada ya fani ya kilimo cha mboga matunda na maua (Horticultural Crops), Zana za Kilimo, Uzalishaji wa Mazao, Umwagiliaji na Huduma za Kiufundi, Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi ya Kilimo na Chakula na Lishe.

Aidha, Wahitimu hao wanauwezo wa kiutendaji katika kuanzisha na kutunza bustani za mimea, mboga na matunda, kushauri wakulima kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo TEHAMA, kusimamia kazi zote zinazohusu matumizi ya Zana za Kilimo na kuzifanyia matengenezo kila itapohitajika, kujenga miundombinu ya shamba ikiwemo maghala, vihenge na mabanda ya wanyama mbalimbali.

Pia wanauwezo wa kuzalisha mazao makuu ya chakula na biashara yanayolimwa nchini, kusaidia tafiti na kukusanya takwimu za utafiti wa mazao, kusimamia ujenzi wa miradi midogo ya umwagiliaji na kuandaa michoro ya miradi hiyo.

Wahitimu hao pia wanao uwezo wa kuandaa mazao baada ya kuvunwa, kuchakata na kufungasha, kufanya tathmini ya lishe na mahitaji ya chakula katika jamii, kuandaa mipango na kutoa ushauri kwa jamii kuhusu masuala ya lishe.

Serikali inawafahamisha Wadau wa maendeleo ya kilimo na mifugo, Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na yeyote mwenye mahitaji yanayoweza kutekelezwa na wataalam hawa kuwa wanayo fursa ya kuwaajiri, wahitimu hao ili kupata ufanisi katika shughuli zao za kilimo.

Imetolewa na;
                                  
          Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
         WIZARA YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI

 19/01/2016
Posted by MROKI On Monday, January 18, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo