Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwonyesha Kaimu Meneja wa
Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abel Mhanga (kulia) orodha ya makontena 2,431
yaliyopitia kwenye banda ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi wakati alipofanya
ziara kwenye bandari hiyo Disemba 3, 2015.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu utoaji
bili za kulipia kodi za serikali kwa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam
kutoka kwa ofisa mwandamizi wa masuala ya fedha, Sartho Mbuya wakati
alipotembelea bandari hiyo Disemba 3,
2015 kutaka kujua ukweli wa tuhuma za makontena 2431 yaliyopita bandarini hapo
bila kulipiwa kodi za serikali.
************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara nyingine ya
kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji
wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila
kulipiwa ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari
ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi
kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa
kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na
kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali
mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga
amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo
ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa
mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa
kielektroniki (e-payment).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2015), wakati
akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo
unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifestmoja
ikisema kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya
umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben
Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo
cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs
ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo
zilizoandikishwa kwenye manifest.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akitembelea stesheni ya reli ya
Dar es Salaam Disemba 3, 2015.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi
za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na
baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu
kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias Mshana,
Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi
lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni
13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. “Nia ya
kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara
lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.
“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka
benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya miradi,
fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo
wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.
Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa
TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko
ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia
Julai – Novemba 2014.
Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi Mshana asimamie
uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata
mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua
aina ya usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari
wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia
mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L.
P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, DESEMBA 3, 2015.
0 comments:
Post a Comment