MIONGONI mwa vitu ambavyo huwa si vipendi na
huniumiza ni migogoro baina ya mkulima na mfugaji sehemu yeyote ile nchini.
Katika hali ya kawaida mkulima na mfugaji ni mtu mmoja, kwa uhalisia wa kawaida hasa katika vijiji tulivyozaliwa na kukulia. Vijijni ni lazima ufuge kuku au mbuzi kama si Ng'ombe.
Huenda hii inanitokea kwakua nami nimezaliwa
katika nyumba ya mkulima lakini pia aliyekuwa anafuga mifugo mingi tu kipindi
hicho lakini kwa sasa imebaki historia kutokana na wizi uliokuwa umekithiri wa
mifugo kipindi hicho.
Mbaya zaidi migogoro mingi baina ya mkulima na
mfugaji inatokea mara kwa mara Mkoani Morogoro tena Wilaya ya Mvomero ambayo
tena mimi ni mkazi wake na mzaaliwa wa Wilaya hiyo nikitokea pale Kijiji
cha Kinyenze, Kata na Tarafa ya Mlali.
Binafsi nilishuhudia mara kadhaa wazazi wangu
wakilipa faini baada ya mifugo yetu kula mazao ya watu pindi ikienda malishoni
na wakati mwingine ni mimi nilihusika nilipokuwa nachunga.
Namshukuru Mungu sana kwani matukio hayo yalikuwa
yakitokea mara chache na majirani zetu walikuwa ni watu waungwana sana kwani
mbali na kulipa faini hakuna baya zaidi ambalo lilikuwa likitokea kipindi hicho
zaidi ya baba kumkata mshahara mchungi au mimi kulamba mijeledi kwa kuachia Ng'ombe au Mbuzi wakala mazao ya watu.
Hali siku hizi ni tofauti kabisa wafugaji na
wakulima wa siku hizi nadhani wamekuwa wakorofi na kutotaka suluhu pindi
matatizo kama hayo yanapotokea.
Lakini pia si wakulima na wafugaji tu, viongozi wetu hasa wa kisisiasa nao huchangia kwa kiasi fulani kutokea kwa migogoro hii baina ya makundi haya mawili katika jamii.
Mwanasiasa katika kutaka kulinda kura na maslahi yake ya kuendelea kutawala na kuonekana mwema, huenda na kuwahakikishia kuwa kundi moja kuwa hapa ni kwenu na hugeukia kundi lingine na kusema hapa ni kweni sasa kila mmoja akijazwa jeuri matokeo yake mwisho wa siku ni kukamatana mashati. KUSOMA ZAIDI POROJO HII BOFYA HAPA
Juzi vyombo vya habari viliripoti juu ya mapigano baina
ya wakulima na wafugaji yaliyotokea Kijiji cha Dihinda Kata ya Kanga Wilaya ya
Mvomero Mkoa wa Morogoro ambapo mkulima mmoka aliuwawa kwa mkuki na Ng’ombe 71
kukatwa mapanga na kufa.
Aidha, katika tukio hilo lililotokea Desemba 12,
watu wanne akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Polisi walijeruhiwa na wamelazwa
katika Hospitali ya Misheni ya Bwagala mjini Turiani wakiendelea kupatiwa
matibabu.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Rajabu Kilama alisema
mapigano hayo yalitokea baada ya ng’ombe 162 kuingia katika shamba la kunde la
Bakari Mlunguza na kuharibu zao hilo.
Hii si mara ya kwanza kutokea kwa mapigano ya aina
hiyo Wilayani Mvomero na mara kwa mara imekuwa ikitokea katika vijiji vya
Kambala, Merela na Mgongolwa na mara zote kama si vifo vya wakulima basi ni
majeruhi na vifo vya mifugo.
Mapigano hayo yamekuwa si yakipooteza uhai wa watu
lakini hofu inayokuwepo miongoni mwa wananchi dhidi ya makundi mengine imekua
ikiathiri uzalishaji mali.
Wananchi wamekuwa wakishindwa kwenda mashambani
kulima kuhofia kushambuliwa na wafugaji, lakini pia wanafunzi nao wakishindwa
kwenda shule, hivi sasa wananchi wa Kijiji hicho cha Dihinda wamekihama
kutokana na hofu.
Licha ya tawala zilizopita nchi hii nazokutoa
ahadi za mara kwa mara za kumaliza migogoro hiyo lakini pia Rais John Magufuli
nae katika kipindi cha kampeni aliahidi kumaliza tatizo hilo na kutoa salamu
kwa watendaji atakao wachagua yeye wakishindwa kumaliza migogoro hiyo nini
kitawapata.
Septemba 30 mwaka huu, Magufuli akihutubia wakazi
wa Kibaigwa wilayani Kongwa katika Mkoa wa Dodoma, alisema viongozi atakaowateua kuanzia makamanda wa
polisi, wakuu wa wilaya na mikoa, wawe macho vinginevyo, ikitokea mapigano
katika maeneo yao, hawatakuwa na kazi.
“Viongozi nitakaowateua wawe wakuu wa mikoa, wakuu
wa wilaya, katibu tarafa, makamanda wa polisi wa mikoa, wakuu wa polisi wa
wilaya ikitokea mapigano kwenye eneo lake, siku hiyo kazi anaondoka nayo,”
alisema Magufuli.
Sitaki hii leo kuwachongea viongozi wote ambao
walichaguliwa na Rais waliopo hapo Mvomero na mkoa wa Morogoro kuwa wameshindwa
kudhibiti mapigano katika eneo lao bali ni kuwakumbusha kutembelea maeneo hayo
mara kwa mara na kusikia kero zilizopo kutoka kwa wananchi.
Naimani kuwa kabla ya mapigano kutokea ipo hali ya
muda mrefu ya mvutano baina ya pande hizo mbili na yanapozidi ndio
ushambuliana.
Hivyo mamlaka zilizopo Mvomero kama zitajenga
utamaduni wa kupata taarifa za mara kwa mara zinazotokea huko vijijini basi ni
rahisi kutatua migogoro hiyo mapema kuliko kusubiri yatukie ndipo watoe pole.
Nivyema sasa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba
kukaa chini na kuandaa mikakati madhubuti kwa kushirikiana na watendaji wote wa serikali na wananchi ili
kunusuru mapigano mengine kutokea.
Mkakati huo uwe shirikishi na usilenge tu Mvomero
bali nchi nzima ili kumaliza kabisa mapigano ya namna hiyo yanayoweza kutokea
nchini.
0 comments:
Post a Comment