Nafasi Ya Matangazo

September 17, 2015

Mwenyekiti wa Tamasha la 34 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni, John Mponda (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 27, 2015 katika Kumbi na Viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), mkoani Pwani. Kulia ni Katibu wa Tamasha hilo na Ofisa Biashara, Benjamini Malimbali na Ofisa Habari, Sophia Mtakajimbo.
Hapa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, John Mponda (kulia) akisisitiza jambo kuhusu tamasha hilo. Kushoto ni Ofisa Habari wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
 Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

TAMASHA la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo liliasisiwa mwaka 1981 na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho kwa sasa ni Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo. Lengo kuu la Tamasha kwa wakati huo ilikuwa ni kuwapa nafasi wanafunzi wa chuo cha sanaa kuonyesha kwa vitendo yale waliojifunza kwa mwaka mzima kwa kuwashirikisha wakazi wa Bagamoyo, baada ya Tamasha hilo kufanikiwa uongozi wa chuo uliamua tamasha hilo lifanyike kila mwaka kwa kushirikisha Vikundi mbalimbali vya ndani na nje ya nchi ili kubadilishana Uzoefu  na hivyo kujizolea umaarufu ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo mwaka huu litafanyika kwa mara ya 34 kuanzia tarehe 21-27 Septemba katika kumbi na viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambao ndio wenyeji na waandaaji wa tamasha hilo kongwe Tanzania.

Maandalizi yote ya Tamasha hili yamekamilika Tamasha la mwaka huu linabeba Kauli mbiu isemayo ‘SANAA NA UTAMADUNI KATIKA UCHAGUZI HURU NA WA AMANI’  Aidha kutakuwa na mada ndogondogo zitakazotolewa kupitia kongamano na warsha zitakazohusu  Haki za binadamu, Rushwa na kupinga Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Tamasha atakuwa mzee Rashid Masimbi, aliyekuwa mkuu wa chuo wa kwanza toka taasisi ilivyokuwa chuo cha sanaa,hivyo kwa kutambua mchango wake kwenye sanaa Taasisi imempa heshima ya kuwa mgeni rasmi .

Tamasha la mwaka huu litahusisha Ngoma za Asili, Maigizo, Sarakasi, Mazingaombwe, Muziki wa kisasa na asili, Sanaa za Ufundi  na bidhaa mbalimbali.

Jumla ya vikundi 65 kutoka ndani na nje ya Tanzania vimethibitisha kushiriki,ambapo vikundi 59  ni kutoka ndani ya Tanzania na vikundi 6 kutoka nchi za Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Korea na Congo na Zimbabwe.

Kiingilio kwenye tamasha kwa wakubwa shilingi 3000/=,kwa watoto shiling 1000/= na kwa wageni wasio watanzania  shilingi 5000/=

Taasisi inatoa wito kwa wadau mbalimbali wa Sanaa,Makampuni,Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kujitokeza kudhamini tamasha hili muhimu ambalo hufanyika kila mwaka ili kulifanya liwe bora na la kimataifa zaidi , kwa mustakabali wa sanaa na utamaduni wa Mtanzania. 

(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Posted by MROKI On Thursday, September 17, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo